***
YATOKANAYO NA TAMASHA LA JINSIA LA 7 NGAZI YA WILAYA Tarehe 27 –29 Agosti, 2024- Wilaya ya Kondoa, Dodoma
Kauli mbiu: “Dira Jumuishi ya 2050: Miaka 30 Baada ya Beijing Tujipange”
Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kwa kushirikiana na mashirika yanayotetea haki za wanawake na usawa wa jinsia nchini, Vituo vya Taarifa na Maarifa, na washiriki wa semina za Jinsia na Maendeleo (GDSS), kwa ufadhili wa wadau mbalimbali wa maendeleo wakiwemo Ubalozi wa Uswidi, CrossRoads International UN Women, Coady international, Ubalozi wa Ireland, Ubalozi wa Canada kupitia Seedchange na Aga Khan Foundation, umefanya Tamasha la 7 la Jinsia ngazi ya Wilaya. Tamasha hili limefanyika hapa katika Viwanja vya Sabasaba, Wilaya ya kondoa, Mkoani Dodoma kuanzia tarehe 27-29 mwezi wa Agost 2024.
Tamasha hili limeongozwa na mada kuu isemayo, ‘“Dira Jumuishi ya 2050: Miaka 30 Baada ya Beijing Tujipange”, huku mada ndogo ndogo zikiangazia Miaka 30 ya 30 ya Beijing: wako wapi viongozi; rasilimali za taifa ziwanufaishe wananchi wa pembezoni; Harakati za kijamii na ushiriki wa makundi rika; Teknolojia, mabadiliko tabia nchi, masuala ya ukatili wa kijinsia; pamoja na masuala ya kazi zenye ujira na staha kwa wanawake na vijana.
Tamasha hili la 7 la Jinsia ngazi ya Wilaya limekutanisha zaidi ya washiriki 300 wanaojumuisha wadau wa maendeleo (SeedChange, na Aga Khan Foundation), asasi za kiraia zikiwemo WFT, CAMFED, WAJIBU, Chuo cha Serikali za Mitaa- Hombolo, Policy Forum, PELUM Tanzania, na Msichana Initiative, vikundi vya kijamii, vikiwemo vituo vya taarifa na maarifa kutoka Mtwara Vijijni, Kondoa Vijijini, na Kishapu, Lindi, Same, Mwanga, Babati, Morogoro Vijijini, Gairo, Kinondoni, Ilala, na Ubungo, na wanaharakati ambao wamekuwa bega kwa bega na TGNP katika kuchagiza usawa wa jinsia. Serikali ya Jamhuri ya Tanzania imeshiriki kupitia ofisi ya Mkoa wa Dodoma, Wilaya ya Kondoa na Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa.
Katibu wa Kituo cha Taarifa na Maarifa Haubi, Anna Ambrosi ambao ni wenyeji wetu, alieleza uhusiano wa kazi za vituo vya taarifa na tamasha la Jinsia. Tamasha la jinsia ni kilele cha harakati za ngazi ya jamii, ambapo katika tamasha la jinsia ngazi ya wilaya wanajamii wa vituo vya taarifa kutoka wilaya mbalimbali hapa nchini wanashirikishana uzoefu wao katika masuala mbalimbali yanayohusu usawa wa kijinsia, mafanikio yao, mbinu walizotumia kufikia mafanikio hayo, changamoto wanazokabiliana nazo na kuweka mikakati ya pamoja ya kupambana na changamoto hizo na kuendeleza harakati katika ngazi ya jamii ili kufikia usawa wa kijinsia katika jamii zao.
Mkurugenzi wa TGNP, Bi. Lilian Liundi alitoa usuli kuhusu Tamasha la Jinsia la ngazi ya wilaya ikiwa ni muendelezo wa mkakati wa taasisi tokea mwaka 1996 kuunganisha sauti ya pamoja na kutekeleza mikakati ya kufikia usawa wa kijinsia. TGNP imefanya matamasha 15 ya kitaifa ambapo yameweza kuleta pamoja zaidi ya washiriki 30,0000 (70% wanawake na 30% wanaume) moja kwa moja na zaidi ya Milioni 15 kupitia mitandao mbalimbali. Pia, jumla ya matamasha 6 ngazi ya wilaya; na moja ngazi ya Kanda yamekwisha fanyika na kuwafikia watu 7000, ambapo asilimia 70 ya washiriki wake ni wanawake na asilimia 30 ni wanaume na kushawishi maabadiliko. Kwa mwaka huu ndo tumefanya tamasha la 7 la jinsia ngazi ya wilaya. Hivyo, Tamasha limekuwa sehemu ya kuendelea kutanua harakati za ujenzi wa nguvu za pamoja nchini na kutoa fursa kwa watu wengi zaidi kushiriki.
Mwenyekiti wa Bodi ya TGNP, Bi. Gemma Akilimali aliweza kudadavua kwa kina Mada kuu ya Tamasha hili. Tamasha hili limetumika kama jukwaa la kutuwezesha kutafakuri kwa kina kuhusu utekelezaji wa Azimio na Mpangokazi wa Beijing, ambao unatimiza miaka 30. Baada tu ya Azimio la Beijing, nchini Tanzania kulikuwa na fursa ya kuandaa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025, hivyo ilikuwa ni fursa nzuri sana ya kuingiza masuala ya kijinsia katika Dira hii.
Na ukiangalia katika Dira hii, masuala ya Jinsia yaliweza kuingizwa kwa kiwango Fulani. Tunapotafakari miaka 30 ya Beijing, nchi yetu pia ipo katika mchakato wa kuandaa Dira ya taifa ya maendeleo 2050, hii ni fursa nyingine adhimu ya kuhakikisha kuwa Dira hii ya 2050 inaingiza kwa wingi masuala ya kijinsia.
Mwaka huu pia, pamoja na mchakato wa kuandaa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, nchi yetu pia itakuwa na mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu 2024 na uchaguzi mkuu mwakani 2025, hivyo, wito wetu mkubwa ni ongezeko la ushiriki wa wanawake katika ngazi mbalimbali za maamuzi na uongozi. Tamasha hili limetupa fursa ya pekee ya kutafakari maeneo haya matatu ya mada kuu ya tamasha ambayo yana mahusiano makubwa sana.
Mgeni Rasmi wa Tamasha hili la 7 la Jinsia Ngazi ya Wilaya, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mheshimiwa Rosemary Senyamule katika neno la ufunguzi alitambua mchango wa TGNP katika kuendeleza harakati za usawa wa kijinsia tangu mwaka 1993 katika ngazi zote za kitaifa hadi katika ngazi za kijamii (kata) ili kuhakiksha walengwa hasa wanaohitaji elimu hii waipate, akitolea mfano kata ya Haubi ambayo alisema ni moja ya kata zinazohitaji sana elimu hiyo ya usawa wa kijinsia.
Aidha, alihamasisha wanakondoa kutumia fursa hii adhimu ya tamasha kutoa maoni yao kupitia eneo maalumu kwa ajili ya kukusanya maoni ya wananchi kwa ajili ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050. Aliwataka pia wananchi kupenda kuhudhuria mikutano ya serikali ili kuweza kutambua fursa mbalimbali zilizopo serikali na kuweza kunufaika nazo, akitolea mfano wa uwepo asilimia 10 ya mapato ya halmashauri inayotengwa kwa ajili ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, pamoja na uwepo wa dirisha la asilimia 30 ya zabuni za serikali kwa ajili ya kupewa makundi maalumu ikiwemo wazabuni wanawake, na watu wenye ulemavu.
Hii ni kwa mujibu wa sheria yam amla ya usimamizi wa ununuzi wa umma (PPRA) sura namba 410 ya mwaka 2023 kifungu cha 64 kinachotaka Halmashauri na ofisi zote za serikali kutenga bajeti ya ununuzi kila mwaka kwa ajili ya wazabuni wanawake, vijana na makundi maalumu.
Katika hotuba yake pia alifafanua dhamira ya serikali kugharamia matibabu ya wanawake wajawazito ambao wanawajibika kuleta nguvu kazi ya taifa na kusistiza kuwa mtumishi yeyote anayekiuka maagizo hayo ni muhimu wananchi watoe taarifa kwa mamlaka husika na aliweza kutoa namba ambazo zinaweza kutumika kutolea taarifa ukiukwaji wa maagizo hayo ya serikali kwa taasisi na watendaji wa vituo vya umma vya huduma za afya.
Mgeni Rasmi pia aliweza kutoa Tuzo ya Heshima ya Marehemu Mama Mercelina Fwaja kwa familia yake kama sehemu ya kumuenzi, kusherekea na kutambua mchango wake katika kuanzisha harakati kondoa. na ambaye alitoa mchango mkubwa sana katika kuanzishwa na kuratibiwa kwa mitandao ya kijnsia ya kati (IGNs) hapa Kondoa, IGNs hizo zilitumika kuleta vuguvugu la ukombozi wa wanawake na usawa wa kijinsia katika wilaya mbalimbali nchini kwa kipindi hicho.
Mercelina alijenga vuguvugu la harakati ambalo halikuishia katika mitandao ya kawaida ndani ya jamii, bali iliingia hadi kanisani, ambapo Askofu alimchukua Mercelina kuwa mwenzeshaji na mhamasishaji wa WAWATA katika Wilaya ili aweze kuelimisha masuala haya ya kijamii, utunzaji wa Watoto na kuwajali wagonjwa.
Kutokana na kazi hizo, Mercelina aliweza kuonesha uzoefu, nguvu na ujasiri wake, ambao ulimfanya aende kuwakilisha wanawake wa mashinani katika mkutano wa Umoja wa Afrika (AU) Addis Ababa, Ethiopia. Baadae, pia aliteuliwa kwenda Washington, Marekani kwenye Mkutano wa Umoja wa Mataifa, wakati Mheshimiwa Asharose Migiro akiwa uko kama balozi wa Tanzania.
Katika siku ya pili ya Tamasha, washiriki walijikita kwenye tafakuri na mijadala kupitia warsha zilizoangazia maeneo muhimu manne (5): Miaka 30 ya 30 ya Beijing: wako wapi viongozi; rasilimali za taifa ziwanufaishe wananchi wa pembezoni; Harakati za kijamii na ushiriki wa makundi rika; Teknolojia, mabadiliko tabia nchi, masuala ya ukatili wa kijinsia; pamoja na masuala ya kazi zenye ujira na staha kwa wanawake na vijana. Warsha hizi zilitanguliwa na mjadala wa wazi uliojikita katika kutathmini Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 na maandalizi ya Dira ya 2050.
Katika utekelezaji wa Dira 2025, kuna maeneo ambayo tumepiga hatua. Eneo la kwanza ni uzingatiwaji wa masuala ya kijinsia katika sera za kisekta, sheria na program, ikiwemo Sera ya huduma za kijamii- Sera ya Maji (2002); Sera ya Elimu na Mafunzo (2014); na Sera ya Afya (2007). Sheria ya Majisafi na Usafi wa Mazingira, Sura ya 272; Sheria ya Ununuzi wa Umma, Sura ya 410; Sheria ya Fedha ya Serikali ya Mitaa, Sura ya 290;
Haya yamepelekea kupata mafanikio kama ongezeko la upatikanaji wa maji umeongezeka kutoka asilimia 50 mwaka 2000 mpaka 86.7kwa mwaka 2020 kwa upande wa mijini, wakati upande wa vijijini, imetoka asilimia 55 mwaka 2000 hadi 72.3 mwaka 2020. Hata hivyo, hali halisi inaonesha kuwa miundo mbinu imeongezeka ila upatikanaji wa maji pale yanapohitajika hayapatikani- Bomba si maji. Tumeona ongezeko la idadi ya wafanyakazi wanawake katika wizara ya maji, hadi kufikia mwezi April 2024 wanawake walikuwa ni asilimia 60 ya wafanyakazi wa wizara ya maji, ambao ni sawa na wafanyakazi 5663. Hata hivyo, changamoto ni kwamba ni asilimia 24 tu kati ya hao wanawake, ambao ni sawa na nafasi 201, wapo katika ngazi ya maamuzi. Idadi hii ni ndogo sana.
Kwa upande wa afya imesaidia kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi nchini kutoka vifo 578 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2004/05 hadi kufikia vifo 238 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2022/23. Kwa vifo vya Watoto chini ya miaka 5 kutoka 43 kwa vizazi hai 1000 mwaka 2015/16 hadi vifo 36 kwa vizazi hai 1000 mwaka 2022/23.
Hata hviyo, katika mijadala yetu tumeona kuwa wanawake wanaoleta nguvu kazi wanalazimika kugharamia huduma za kujifungua kinyume na ahadi ya serikali. Elimu ya afya ya uzazi kwa elimu rika hususani kwa vijana wa rika balehe bado haijatosheleza, kwa upande wa maeneo ya vijijini bado hiyo elimu haijawafikia. Kwa upande wa kondoa, tumepokea visa vya vitendo ukatili wa kijinsia bado vipo juu, ikiwemo ndoa za utotoni, ulawiti, ubakaji, ukeketaji na vipigo kwa wanawake bado zipo kwa kiwango cha juu kutokana na mila na desturi na misingi ya dini. Kadhalika, tumeona kwamba sababu nyingine inayochangia matukio ya ukatili wa kijinsia ni ongezeko la mmomonyoko wa maadili kwenye jamii zetu zinazochangiwa na uwepo wa ajira zisizo na staha kwa wanawake na kazi zisizo halali. Kwa hapa kondoa, kumekuwa na changamoto ya ulevi uliokithiri na matumizi ya bangi ambayo yanapelekea athari kubwa kwa Watoto na vijana kwa baadhi ya maeneo.
Kwa upande wa masuala ya kiuchumi, tumeona uingiwaji wa masuala ya kijinsia kwenye sera kama vile Sera ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo (2003); Sera ya Taifa ya Kilimo (2013) pamoja na Sera ya Taifa ya Mazingira (2021); na Sera ya Taifa ya Huduma ndogo za Fedha (2017). Hatua hizi zimeepelekea kuwepo kwa fursa mbalimbali za kiuchumi kwa wanawake, vijana na makundi maalumu kama uwepo asilimia 10 ya mapato ya halmashauri inayotengwa kwa ajili ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, pamoja na uwepo wa dirisha la asilimia 30 ya zabuni za serikali kwa ajili ya kupewa makundi maalumu ikiwemo wazabuni wanawake, na watu wenye ulemavu; Mikopo ya kilimo kupitia benki ya taifa ya kilimo pamoja na programna u ya kesho iliyo bora (BBT); pamoja na mifuko mingine 19 ya uwezeshaji wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kiuchumi katika viwanda na biashara.
Hata hivyo, tumeona kwamba bado kuna upungufu au ukosefu wa upatikanaji wa taarifa hizi za fursa, ikiwemo wanakondoa, na wakati mwingine kumekuwa na taarifa zisizo sahihi au zinazochanganya. Hivyo, kuwa ni changamoto kwa makundi haya kunufaika na fursa hizi zilizopo. Licha ya kuwepo kwa fursa Nyingi za kiuchumi, tumeona kwamba bado wanawake wanawake wanaendelea kuelemewa na mzigo mkubwa wa kazi zisizo na ujira inayopelekea kuwapunguzia muda wa kujishughulisha na shughuli za uzalishaji mali, ambazo zinaweza kuwaingizia kipato.
Kwa upande wa uwakilishi na ushiriki katika ngazi za maamuzi, kwa hapa Kondoa tumeona bado kuna changamoto, wanawake hawashiriki vya kutosha katika michakato ya uibuaji wa fursa na vikwazo vya maendeleo na mikutano ya kusomewa mapato na matumizi katika ngazi ya vijiji/mitaa na kata, na wale wanaoshiriki hawachangi vya kutosha kutokana na mila na desturi na misingi ya dini kandamizi.
Suala la mabadiliko tabia nchi ni janga la kidunia, na tanzania sio kisiwa. Bado uelewa mdogo juu ya tabia ya nchi, teknolojia na kijinsia, na uwekezaji wetu katika kuzuia na kukabiliana na athari za mabadiliko tabia nchi bado ni mdogo. Kwenye kilimo , tumeona kwamba licha ya kwamba kuna ongezeko la wanawake wanaomiliki ardhi kwa ajili ya shughuli za kilimo bado kuna changamoto katika kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao kutokana na ardhi kuwa zimechoka, mbegu zinazotumika katika uzalishaji ni za gharama kubwa na haziwezi kutumika zaidi ya mara moja. Pia, kuna upungufu wa taarifa zinazowasaidia wanawake wakulima kuyafikia masoko ya kimakakati kwa ajili ya mazao yao, ambao wanalazimika kuuza mazao yao yakiwa shambani na hivyo kuuza kwa gharama ambazo si za soko. Kwa baadhi ya maeneo ya kondoa kumekuwa na ucheleweshaji wa pembejeo za kilimo(Mbegu na Mbolea).
Kutokana na changamoto hizo, washiriki wa tamasha hili wametoka na mapendekezo yanayohusisha uwajikaji wa serikali, wadau wa maendeleo na wanajamii ikiwemo:
Kwa serikali:
1. Iwaongezee mamlaka za maji bajeti za kuhakikisha kuwa maji yanasambazwa na yanapatikana wakati wote katika miundo mbinu iliyopo, hasa maeneo ya vijiji vya ndani ndani. Bajeti yam aji bado haijapewa kipaumbele ni azidi asilimia moja ya bajeti kuu. Pia, tunapenda kuona kwamba wilaya na halmashauri zetu zinatengewa fedha za kutosha za kutekeleza afua za kutoa elimu ya afya ya uzazi kwa kundi rika balehe. Aidha, tunapenda serikali itenge bajeti kuwawezesha afisa maendeleo kufikia vijiji mbalimbali kuwaelimisha taarifa za fursa zilizopo na namna wanaweza kuzitumia ili kunufaika nazo.
2. Tunashauri ongezeko la wanawake katika ngazi za maamuzi kwenye sekta ya maji kuanzia kwenye kata hadi taifa. Tunaomba Wilaya hii ya Kondoa kuwa ya mfano katika kuhakikisha kuwa wanawake wanazidi idadi ya wanaume wanaoshika nafasi za mamuzi katika ngazi zote za maamuzi katika sekta ya maji.
3. Serikali ya mkoa wa Dodoma iimarishe usimamizi wa utekelezaji wa agizo la serikali la matibabu bure kwa wanawake wanaojifungua kwa kutoa hizo namba na namna ya kutoa taarifa za ukiukwaji kwenye zahanati, vituo vya afya, hospoitali, na serkali za vijiji.
4. Tunashauri halmashauri zitengeneze mwongozo wa maadili wa uendeleshaji na usismamizi wa shughuli za baa, klabu n.k ili kuepuka kuendeleza vitendo vya udhalilishaji wa wanwake na wasichana vinavyofanyika katika maeneo hayo.
5. Tungependa kuona kwamba mitaala yetu ya elimu inabadilika kwa kutumia lugha, picha na mifano inatumika mashuleni wakati wa kufundisha haikandamizi jinsi moja.
6. Tunashauri serikali ishirikiane na wadau kuhakikisha kuwa wakulima wetu wanapata elimu ya mabadiliko tabia nchi na teknolojia mbalimbali zinaosaidia katika kuzuia na kukabiliana na mabadiliko tabia nchi. Kwa mfano kwa upande wa kondoa, kutokana na ardhi kuwa imechoka, na ikiwekwa mbolea inahamishwa wakati wa mvua, wameanza kutumia teknolojia ya mbegu 9 na jembe la kondoa; na upande wa mamire, wamekuwa wakitumia kilimo ikolojia.
7. Kuwawezesha maafisa ugani na vyama vya ushirika kuhakikisha kwamba wanawafikia wakulima wote na taarifa sahihi za fursa za masoko kwa wakati.
Kwa wananchi.
Vikundi, vituo vya taarifa na maarifa , wanajamii na vyombo vya Habari kwa pamoja , tushirikiane kuhakikisha kwamba tunapoelekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, vitendo vya ukatili wa kijinsia katika ngazi yoyote ile vinatolewa taarifa kwa mamlaka husika kwa wakati na hii iendelee hata baada ya michakato ya uchaguzi.
Tuhamasishane kuongeza ushiriki wa wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu katika vikao vya kimaamuzi kuanzia katika ngazi ya Kijiji, na kata; na kupaza sauti za madai yenye tija kwa makund maalumu.
Tunahamasisha wananchi kuchukua hatua ya kutafuta taarifa za fursa mbalimbali zilizopo.
Kikubwa pia tuimarishe malezi katika ngazi ya familia yanayoelekeza katika kuimarisha usawa wa kijinsia, maadili katika jamii pamoja na uwezeshaji wa kiuchumi.
Katika siku ya tatu ya Tamasha, ambayo ni leo, washiriki wamewasilisha mikakati ya utekekelezaji wa mapendekezo yaliyoibuliwa kutoka kwenye warsha hizo tano kwa kuzingatia hali halisi kwenye kwenye maeneo wanayotoka, rasilimali zinazowazunguka na kwa kupitia nguvu za pamoja, ikitambua umuhimu wa kushirikiana na viongozi wa mila, dini na wa Serikali katika ngazi ya vijiji, kata na Halmashauri.
Taarifa hii imeandaliwa na:
Idara ya Habari,
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP
0 Comments