Ticker

6/recent/ticker-posts

TAWA YATIA SAINI MIKATABA YA UWEKEZAJI WA MIUNDOMBINU YA UTALII

-YATARAJIA KUIINGIZIA SERIKALI ZAIDI YA BILIONI 27 KWA MWAKA

-Zipline, Loji zenye hadhi ya nyota 5 na Kambi za Kitalii zenye hadhi ya nyota 4 kujengwa

Na. Beatus Maganja

MAMLAKA ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA leo Agosti 24, 2024 imetia saini mikataba minne (4) ya uwekezaji wa miundombinu ya utalii na kampuni za Sea and Bush Ltd na Ritungu Tours and Safaris Ltd Katika mapori ya Akiba ya Kijereshi, Pande na Swagaswaga na eneo la Makuyuni.

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini wa mikataba hiyo iliyofanyika kwenye ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TAWA Mej. Jen. (Mstaafu) Hamis R. Semfuko amesema kusainiwa kwa mikataba hiyo ni sehemu ya jitahada za TAWA katika kuunga mkono kwa vitendo maono ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kukuza na kuendeleza biashara ya utalii nchini.

Semfuko amesema kupitia uwekezaji huo, TAWA inatarajia kuingizia Serikali mapato ya wastani wa Shillingi Bilioni 27.3 kwa mwaka. Aidha, amesisitiza kuwa Bodi yake imejipanga kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa mikataba hiyo ili kuleta tija iliyokusudiwa katika kukuza utalii na uwekezaji katika tasnia ya utalii nchini.

Aidha, Mwenyekiti huyo ameahidi kuwa Bodi yake itawapa ushirikiano stahiki wawekezaji wote ili kuhakikisha wanafikia malengo yao ya uwekezaji katika maeneo yanayosimamiwa na TAWA.

Vilevile, Semfuko amesema kuwa Bodi ya Wakurugenzi ya TAWA ina matarajio ya kuona uwekezaji huo ukisaidia kuboresha miundombinu ya utalii, kutoa ajira kwa watanzania na kuboresha maisha ya jamii inayozunguka maeneo ya uwekezaji ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea katika maeneo hayo ili kujionea vivutio vilivyopo na kuongeza mapato ya Serikali.

Kwa upande wake Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA, Mabula Misungwi Nyanda amesema katika kuhakikisha kuwa maeneo yanayosimamiwa na Taasisi hiyo yanaongezewa thamani katika kipindi cha mwaka wa fedha 2023/24, TAWA ilitangaza kwa umma fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo katika maeneo yake na kupata jumla ya maombi matano kutoka kwa Kampuni 3 zilizoomba kuwekeza katika maeneo hayo.

Amesema hatua hiyo ililenga kufikia malengo ya Serikali ya kuongeza idadi ya watalii kutoka millioni 1.5 hadi watalii millioni 5 na mapato kutoka dola za Marekani bilioni 2.6 hadi bilioni 6 kwa mujibu wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 2020/2025.

Sanjari na hilo, Kamishna Mabula amesema uwekezaji na kampuni hizo utakuza Utalii kwa kuongeza idadi ya vitanda katika maeneo yanayosimamiwa na TAWA ambapo jumla ya vitanda 360 vitaongezwa na wawekezaji katika maeneo ya uwekezaji kwa kujenga Loji zenye hadhi ya nyota 5 na Kambi za kitalii zenye hadhi ya nyota 4 katika Pori la Akiba Kijereshi na Hifadhi ya Wanyamapori ya Makuyuni na kuanzishwa kwa zao jipya la utalii aina ya "Zipline" katika Pori la Akiba Pande ili kuchochea na kukuza utalii Katika Jiji la Dar es Salaam.

Ujenzi wa Loji na Kambi za Kitalii katika Pori la Akiba Kijereshi (Simiyu) na Hifadhi ya Makuyuni Wildlife Park (Arusha) utafanywa na Kampuni ya Sea and Bush Ltd , huku kujengaa na kuendesha Zipline katika Pori la Akiba Pande (Dar es Salaam) na ukodishaji na uendeshaji wa Hosteli ya Pori la Akiba Swagaswaga (Dodoma) ukitarajiwa kufanywa na Kampuni ya Ritungu Tours and Safaris Ltd.

Post a Comment

0 Comments