Ticker

6/recent/ticker-posts

KAMATI YA KUDUMU BARAZA LA WAWAKILISHI ZANZIBAR YAIPONGEZA TTCL KWA UTEKELEZAJI MIRADI, UTOAJI ELIMU

Na Leandra Gabriel, Dar es Salaam

KAMATI ya Kudumu ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar limepongeza jitihada za Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL,) katika utekelezaji wa miradi ikiwemo kuhakikisha wananchi wanapata huduma za mawasiliano pamoja kutoa elimu kwa shirika la Mawasiliano Zanzibar (ZICTIA.) katika kuhakikisha watanzania wanapata huduma za mawasiliano.

Akizungumza leo wakati wa ziara ya kamati hiyo katika ofisi za Makao Makuu ya Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL,) jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mwanaasha Juma amesema wametembelea TTCL na kujifunza namna wanavyofanya kazi na taratibu za kiutendaji pamoja na kujadiliana namna ya kukabiliana na kutatua changamoto ndani ya taasisi.

“Tumejifunza vitu vingi sana, Zanzibar katika wizara yetu ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi inahusika na usimamizi ikiwemo miundombinu ya TEHAMA na uboreshaji wa miundombinu ya mawasiliano na kwa upande wa Tanzania bara Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kupitia TTCL na wadau wengine wanatekeleza majukumu hayo pia ya kuhakikisha huduma za mawasiliano zinaimarika zaidi.” Amesema.

Aidha kuhusiana na sheria inayoiruhusu TTCL kutoa gawio kwa Serikali Bi. Mwanaasha amesema ikifika hatua hiyo wanaweza kutoa gawio ili fedha hizo zielekezwe katika miradi mbalimbali ya maendeleo itakayowanufaisha wananchi.

Amesema, wamefurahi namna Fedha zinazotolewa na Serikali kwa TTCL pamoja na vyanzo vyao vya mapato zinavyoelekezwa katika miradi mbalimbali ya maendeleo ambapo pia wanafanya kazi kwa upande wa Zanzibar hususani katika mikongo ya Taifa kwa kuhakikisha wananchi wanafikiwa na huduma ya mawasiliano.

Aidha amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Hussein Ali Mwinyi kwa kuweka miundombinu imara na kuhakikisha sekta ya mawasiliano inaleta tija kwa wananchi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL,) CPA. Moremi Andrea amesema; ujio wa kamati hiyo umelenga kujifunza pamoja na kukagua shughuli zinazofanywa na shirika hilo.

“Tumepata fursa ya kutoa wasilisho kwa kamati linalohusu masuala ya kiutendaji, mikakati na biashara na tumepokea maelekezo na menejimenti tutayafanyia kazi….Tunashukuru kwa ujio huu na tutaendelea kushirikiana na wenzetu waliopo upande wa Zanzibar ili kukuza sekta ya mawasiliano.

Wajumbe wa kamati hiyo pia wametembelea Kituo cha Uangalizi na Uendeshaji wa Mtandao (NOMC,) pamoja na Miundombinu ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mwanaasha Juma (kushoto,) akizungumza na waandishi wa Habari wakati wa ziara hiyo na kueleza kuwa wametembelea TTCL na kujifunza namna wanavyofanya kazi na taratibu za kiutendaji pamoja na kujadiliana namna ya kukabiliana na kutatua changamoto ndani ya taasisi. Leo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL,) CPA. Moremi Andrea (kulia,)akizungumza na waandishi wa Habari wakati akipokea ugeni huo na kueleza kuwa  ujio wa kamati hiyo umelenga kujifunza pamoja na kukagua shughuli zinazofanywa na shirika hilo. Leo jijini Dar es Salaam.
Matukio mbalimbali wakati wa hafla hiyo.

Post a Comment

0 Comments