Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mheshimiwa Mwanaasha Khamis Juma akiongea na waandishi wa habari wakati wa ziara ya kamati hiyo ilipotembelea miradi ya ujenzi wa miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) na madaraja ya juu
Meneja wa Mradi wa ujenzi wa miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT), Mhandisi Leonard Ngayungi (mwenye shati ya bluu bahari) akielezea maendeleo ya utekelezaji wa miradi hiyo mbele ya wajumbe wa Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar Agosti 23, 2024. Kulia kwake ni mwenyekiti wa kamati hiyo Mheshimiwa Mwanaasha Khamis Juma
Mhandisi Mshauri katika Mradi wa ujenzi wa miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) Awamu ya Tatu Mhandisi Andrew Burnside kutoka kampuni ya SMEC akielezea maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo mbele ya wajumbe wa Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar Agosti 23, 2024
Wajumbe wa Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar na maofisa kutoka Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) wakitembelea miradi ya ujenzi wa miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT)
Picha mbalimbali zikionesha hatua mbalimbali za ujenzi wa mradi wa miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) katika jiji la Dar es Salaam kama zilivyokutwa na mpiga picha wetu Agosti 23, 2024
**************************
Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Mwanaasha Khamis Juma, Agosti 23, 2024 imetembelea kujionea utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa miundombinu ya ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) pamoja na madaraja ya juu (fly over) ambayo inatekelezwa na Serikali kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) katika jiji la Dar es Salaam,kwa lengo la kujifunza ili maarifa watakayoyapata wakayatumie katika upande wa pili wa Tanzania Zanzibar ambapo kwa sasa ujenzi wa madaraja ya juu visiwani humo umeanza.
Akiongea mara baada ya kutembelea miradi hiyo, Mheshimiwa Mwanaasha amesema, kwa upande wa Zanzibar wameona haja ya kujenga madaraja ya juu kwa lengo la kuondosha usumbufu wa foleni za magari katika maeneo mbalimbali visiwani humo na kwa hivyo kulazimka kuja kujifunza na kujionea utekelezaji wa miradi hiyo kwa upande wa Tanzania Bara.
Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar ameongeza kwa kusema kuwa, wana imani miradi ikikamilika kwa wakati na itaondosha kero ya foleni kama ambavyo kero hiyo ilivyoondoshwa kwa upande Tanzania Bara mara baada ya miradi hiyo kukamilika.
Katika hatua nyingine, ameeleza kuridhishwa na utekelezaji wa miradi ambapo pia ametoa pongezi na shukrani kwa viongozi wakuu wa pande zote mbili za Muungano kwa kuwa na maono na azma ya kuondosha usumbufu ambao wananchi wao wamekuwa wakiupata katika miundombinu ya barabara.
"Tumeona hatua mbalimbali ambazo wenzetu wamezifikia katika utekelezaji wa miradi hii na kuweza kuondosha usumbufu mkubwa unaoletwa na foleni. Kama kamati tumeridhishwa na utekelezaji wa miradi iliyokamilika na inayoendelea" Alisema Mheshimiwa Mwanaasha na kuongeza
"Tunawashukuru viongozi wetu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa maono yao ya kuondosha usumbufu kwa wananchi katika miundombinu ya barabara"
Kwa upande wake Meneja wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) Mhandisi Leonard Ngayungi amesema, kwa sasa kuna miradi mitatu ya BRT ambayo utekelezaji wake unaendelea huku ujenzi wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka Awamu ya Pili (BRT II) ukifikia asilimia 99 ambapo kwa sasa wako katika hatua ya mwisho ya kuukamilisha mradi huo.
"Tuna miradi mitatu ya ambayo utekelezaji wake unaendelea, ujenzi wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka Awamu ya Kwanza (BRT I) umeshakamilika na unaendelea kutumika huku awamu ya pili ya mradi huo kutoka Mbagala hadi Gerezani ukifikia asilimia 99 na tuko katika hatua ya mwisho ya kufunga taa kwa ajili ya usalama na kuongozea magari" alisema Mhandisi Ngayungi na kuongeza
"Kwa awamu ya tatu ya mradi kutoka katikati ya Jiji kwenda Gongo la Mboto umefikia asilimia 59 licha ya changamoto za mvua kuwepo na kuvuruga kidogo utaratibu, lakini mkandarasi ameshajipanga katika kuhakikisha kwamba mradi unakamilika kwa wakati
." Mhandisi Ngayungi ameorodhesha kazi zinazoendelea kwa sasa katika mradi huo kuwa ni pamoja na ujenzi wa mifereji ya maji pamoja na tabaka la chini la barabara huku vituo vya mabasi hayo vikiwa tayari vimeshajengwa.
Vilevile, Meneja huyo wa BRT ametoa pongezi na pia kuishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kuwezesha utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa miundombinu nchini "Tunaishukuru serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha ambazo zinatuwezesha katika kutekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi wa miundombinu nchini.
Naye Mhandisi Mshauri katika mradi wa BRT III kutoka kampuni ya SMEC, Mhandisi Andrew Burnside amesema, mradi huo unaendelea vizuri kwa kuzingatia ubora unaotakiwa huku akikiri kuwa hakuna changamoto zozote kwa sasa zinazowakabili, hivyo wanategemea kukamilisha mradi huo kwa wakati.
Awali, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Ephatar Mlavi akiwa katika ofisi za makao makuu ya Wakala amewaeleza Wajumbe wa Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar kuwa, mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) ulibuniwa kwa lengo la kupunguza msongamano katika jiji la Dar es Salaam, msongamano ambao unapelekea kuathiri shughuli za usafiri na usafirishaji na kwa hivyo uwepo wa mradi wa BRT umechangia kwa kiasi kikubwa kuboresha shughuli za usafiri na usafirishaji katika jiji hilo.
Wajumbe hao wakiwa wameambatana na maofisa kutoka TANROADS wametembelea miradi mbalimbali ya ujenzi wa miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) pamoja na daraja la juu la Kijazi (Kijazi Interchange) na Mfugale
0 Comments