Ticker

6/recent/ticker-posts

IAA KUTOA HUDUMA YA MALAZI BURE KWA WANAFUNZI KAMPASI YA BABATI


Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Prof. Eliamani Sedoyeka amesema baraza la uongozi wa Chuo hicho limeridhia huduma za malazi (accommodation), zitolewe bila malipo kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza, watakaodahiliwa katika fani mbalimbali mwaka wa masomo 2024/2025 katika Kampasi ya Babati.

Prof. Sedoyeka amesema hayo leo tarehe 22 Agosti 2024 katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi awamu ya kwanza Kampasi ya Babati, katika eneo la Waang’waray Mjini Babati mkoani Manyara.

“Nitumie fursa hii kuwakaribisha vijana wote waliomaliza kidato cha nne na kidato cha sita kutoka nje na ndani ya mkoa wa Manyara katika kampasi yetu ya Babati; watapata elimu bora katika mandhari nzuri na huduma ya malazi wataipata bure kabisa,”amesema Prof. Sedoyeka.

Prof. Sedoyeka ameongeza kuwa katika mwaka wa masomo 2023/2024 IAA ilikuwa na jumla ya kozi 72, ambapo kwa ngazi ya cheti ni kozi 16, stashahada 17, shahada 24 na shahada ya uzamili 15, huku akibanisha kuwa mwaka 2024/2025 mitaala tisa itahuishwa na mitaala mipya itaanzishwa kwa kuzingatia mahitaji ya soko la ajira.

Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema IAA imekuwa kwa kasi na kuimarisha nafasi yake kuwa miongoni mwa taasisi za elimu ya juu zinazofanya vizuri na serikali inatambua mchango wake katika kuwaandaa watalaam mahiri kwenye fani za uhasibu, fedha, benki, uchumi, TEHAMA, Usimamizi wa Baishara na nyingine nyingi.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga amehidi kuwa serikali mkoani humo itahakikisha wanafunzi watakaodahiliwa chuoni hapo wanapata huduma zote muhimu na miundombinu hususani barabara kuelekea eneo la chuo inaboreshwa.

Meneja Kampasi ya Babati, Dkt. Eliakira Nnko, amesema Kampasi hii ilianzishwa mwaka 2024 na mwaka huu mwezi Julai imepata ithibati kamili, hivyo kwa mwaka 2024/2025 inatarajia kudahili wanafunzi katika fani za uhasibu, Fedha na Benki TEHAMA, Sayansi ya Kompyuta, Usimamizi wa Biashara, Ununuzi na Ugavi, Uhasibu na TEHAMA, Usimamizi wa Rasilimali watu na Mifumo ya Mawasiliano ya Kompyuta.












Post a Comment

0 Comments