Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba ameongoza ujumbe wa Tanzania kushiriki Mkutano wa 26 wa Kawaida wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (MCO) unaofanyika jijini Lusaka, Zambia tarehe 11 na 12 Julai, 2024.
Mkutano huo ambao ulitanguliwa na Mkutano wa Kamati ya Kudumu ya Makatibu Wakuu wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC uliofanyika kuanzia tarehe 08 hadi 09 Julai 2024, pamoja na mambo mengine umepokea na kujadili agenda mbalimbali zilizowasilishwa ikiwemo Mapitio ya Utekelezaji wa Maamuzi ya Mkutano wa 25 wa MCO na Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC; Hali ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Kanda; na Uimarishaji wa Demokrasia katika Kanda.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano huo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Jamhuri ya Zambia, Mhe. Dkt. Mulambo Haimbe amewakaribisha nchini Zambia wajumbe wa mkutano huo ambao agenda yake kuu ni kutathmini hali ya siasa, ulinzi na usalama katika nchi wanachama wa SADC na kuandaa mikakati ya pamoja ya kuhakikisha amani ya kudumu inapatikana kwenye maeneo ya changamoto.
Aidha, akizungumzia hali ya amani na usalama kwenye maeneo yenye changamoto hususan eneo la Mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Lesotho na eneo la Kaskazini mwa Msumbiji, Mhe. Haimbe amesema hali sasa inatia moyo na kutoa wito kwa nchi wanachama kuendelea kujitolea kwa hali na mali katika kuhakikisha amani, usalama na utulivu wa kudumu vinapatikana kwenye maeneo hayo ili kuwa na maendeleo endelevu ya kiuchumi katika kanda.
Kadhalika amezipongeza misheni za ulinzi wa amani za SADC iliyopo DRC na ile iliyopo Kaskazini mwa Msumbiji kwa kujitoa kikamilifu katika kuhakikisha amani na usalama kwenye maeneo hayo vinarejea mbali na changamoto kadhaa wanazopitia.
Kuhusu misheni ya ulinzi wa amani ya SADC iliyopo Msumbiji (SAMIM) ambayo inamaliza muda wake wa operesheni mwezi Julai 2024, Mhe. Haimbe ameipongeza kwa kazi kubwa iliyofanyika ya kupambana na vitendo vya ugaidi na kurejesha hali ya amani kwa wananchi wa Jimbo la Cabo Delgado lililopo Kaskazini mwa Msumbiji.
“Napongeza misheni ya SAMIM kwa kazi kubwa na nzuri iliyofanyika. Japo wanamaliza operesheni huko Kaskazini mwa Msumbiji, bado mapambano dhidi ya ugaidi na uhalifu wa kuvuka mipaka katika Nchi zote wanachama wa SADC yataendelea. Hivyo naziomba nchi zote wanachana kuendelea kushirikiana na kuandaa mikakati ya pamoja kukabiliana na vitisho hivi” alisisitiza Mhe. Haimbe.
Awali akizungumza, Katibu Mtendaji wa SADC, Bw. Elias Mpedi Magosi amesema kuwa Sekretarieti ya SADC itaendelea kushirikiana na Nchi Wanachama hususan katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zilizopo katika kanda zikiwemo za kiusalama, kijamii na kiuchumi ili hatimaye kuwa na Kanda tulivu kwa ajili ya maendeleo endelevu.
Pia aliongeza kusema bado jitihada za pamoja zinahitajika katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zilizopo katika kanda ikiwemo ugaidi, vitendo vya uhalifu wa kuvuka mipaka na rushwa. Kadhalika, Mhe. Makosi alitumia fursa hiyo kumpongeza Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri anayemaliza muda wake Mhe. Haimbe kwa kazi nzuri aliyofanya katika kipindi chote na kumkaribisha na kumwahidi ushirikiano Mwenyekiti mpya ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Mhe. January Makamba.
Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ilianzishwa mwaka 1996 kwa lengo la kukuza na kulinda amani na usalama katika kanda ya SADC. Tanzania inachukua uenyekiti wa asasi hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia mwezi Agosti 2024.
Mbali na Mhe. Makamba, ujumbe wa Tanzania ulimjumuisha pia Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhe. Daniel Sillo, Katibu Mkuu wa Wizara ya mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Faraji Mnyepe, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Jacob Mkunda, Balozi wa Tanzania nchini Zambia, Mhe. Lt. Jen. Mathew Mkingule, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Kamishna wa Polisi Salum Hamduni, Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Talha Waziri na Maafisa Waandamizi wa Wizara na Vyombo vya ulinzi na Usalama.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba akiongoza ujumbe wa Tanzania kushiriki Mkutano wa 26 wa Kawaida wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-MCO) unaofanyika jijini Lusaka, Zambia tarehe 11 na 12 Julai 2024.
Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Daniel Sillo (kulia) akiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Faraji Mnyepe wakishiriki Mkutano wa 26 wa Kawaida wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-MCO) unaofanyika jijini Lusaka, Zambia tarehe 11 na 12 Julai 2024.
0 Comments