NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
KATIKA kuunga Juhudi za Serikali kwenye Mkakati wa Kitaifa ambao umelenga kuhakikisha Watanzania wanahamia kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia ,Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, kupitia Kitengo Cha Ubunifu na Ujasiriamali kimebuni njia ya kuzalisha nishati safi ya kupikia ya gesi ambayo inatokana na plastiki.
Akizungumza leo Julai 5,2024 Jijini Dar es Salaam katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya kimatifa maarufu kama (SABASABA), Mwanafunzi wa Chuo Kikuu Cha Dar es salaam, Buberwa Laetus amesema wanatumia plastiki za chupa pamoja na nailoni ambazo zinazagaa mitaani kutengeneza nishati ya gesi ya kupikia.
Aidha Laetus ameeleza namna wanavyotengeneza nishati hiyo ambapo amesema kuwa wanakusanya plastiki hizo kisha wanazisaga na kuziweka katika chemba maalumu kwa ajili ya kuyeyusha plastiki hiyo ili kubadilisha kuwa kimiminika.
"Unajua plastiki ukiichoma inatoa vitu vitatu, inatoa gesi, mvuke na kuacha chini vitu vyeusi, tunachoma bila yakuwa na hewa ya Oxygen, tunachukua tu mvuke ambao tunaubadilisha kuwa mafuta"amesema.
Amesema wametengeneza mitungi ambayo inateknolojia ya kubadilisha kimiminika kuwa gesi ambayo ni nishati safi ya kupikia.
Pamoja na hayo Laetus amesema wananchi wamekuwa wakitumia nishati yenye hewa ukaa ambapo wao wameamua kuisaidia jamii kwa kuzalisha nishati safi ya kupikia kupitia plastiki.
Pamoja na hayo amebainisha kuwa nishati hiyo bado haijaingia rasmi sokoni kwa ajili ya matumizi kwani wapo Katika hatua za mwisho kukamilisha mradi huo ili ianze kutumika.
Matumizi ya nishati safi ya kupikia ni agenda mahususi ambayo imechukua nafasi kubwa katika Sera, Mipango na Mikakati ya Serikali mbalimbali duniani. Umuhimu wa agenda hii unasukumwa na ongezeko la uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi pamoja na athari za kiafya zinazotokana na matumizi ya nishati isi-yo safi ya kupikia.
Pia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Sera mbalimbali za kitaifa na kimataifa inatambua umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia kama nyenzo muhimu ya kukabiliana na athari za kimazin-gira, kiafya, kijamii na kiuchumi.
0 Comments