BENKI ya Biashara Tanzania (TCB) imezindua huduma mpya ya akaunti ya kidigitali (TCB POPOTE ACCOUNT ) ambayo itakayomfanya mteja alipie bili mbalimbali kupitia simu yake ya mkononi akiwa sehemu yoyote.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye hafla hiyo ambayo imefanyika leo Julai 30, 2024 katika ofisi za TCB Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Masoko Ukuzaji wa Biashara na Mahusiano ya Umma, Deo Kwiyukwa amesema huduma hiyo ya akaunti ya kidigitali unaweza ukalipia bili mbalimbali na ukanunua tiketi ya treni ya Mwendokasi katika App ya TCB na gharama ya kujiunga na TCB POPOTE ACCOUNT ni shilingi Elfu moja.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Ufumbuzi wa Kigitali wa TCB Jesse Jackson amesema wanatarajia kuwafikia wateja wapya 250,000 ifikapo Desemba mwaka huu kupitia huduma yao ya ‘TCB Popote’ ambayo itawawezesha wananchi kufungua akaunti kidigitali.
“Malengo yetu kwakipindi cha miezi minne iliyobaki tunataka kuwafikia wateja laki mbili na nusu ambao watafungua akaunti hizi zakidigitali kupitia simu janja zao,malengo ya mbele zaidi ambayo yataanzia mwakani ambapo tutakuwa tumeshaweka maandalizi kwa ajili ya simu za kawaida tunatarajia kufikia wateja wengi zaidi,”amesema Jackson.
Pamoja na hayo amesema huduma hiyo ni mwendelezo wa ubunifu unaofanywa na benki hiyo kwakuwa kwa miaka kadhaa TCB imekuwa ikifanya bunifu ili kuleta huduma karibu na wateja.
Amesema lengo lao ni kuwaleta wateja karibu kwakuwa wao ni benki ya tatu kwa matawi na mpaka sasa wana mawakala 6000 Tanzania nzima.
“Tumeona hiyo haitoshi tunahitaji kusogeza huduma za kifedha kwa wananchi kwakuwa takwimu zinaonesha asilinia 89 ya watanzania wanaweza kupata huduma za kifedha ndani ya kilomita tano na asilimia 22 tu ya Watanzania wana akaunti zakibenki,”amesema Jackson.
“Huduma hii ya TCB Popote inafanya mtu anaweza kufungua akunti popote alipo anachohitaji ni simu janja yake na kitambulisho,akaunti hii ikikamilika itaweza kutoa huduma ya kulipia bidhaa mbalimbali na huduma za mikopo,”amesema.
0 Comments