SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) limefanikiwa kushinda tuzo ya utoaji huduma bora katika Maonesho ya 48 ya biashara ya kimataifa Sabasaba ambayo yamefunguliwa leo na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na kukabidhi tuzo hiyo kwa washindi.
Akizungumza mara baada ya kupata tuzo hili Afisa Masoko TANESCO Makao Makuu Innocent Lupenza amesema tuzo hiyo kwao imekuwa na maana kubwa kwani imetambua mchango mkubwa unaotolewa na shirika hilo katika kuhudumia umma hivyo amewashukuru wadau kutambua mchanguo wao katika utoaji huduma bora kwa wananchi.
"Pamoja na changamoto ndogo ndogo ambazo tunaenda kuzimaliza tunafurahi kuona mchango wetu umeweza kutambuliwa",Amesema Lupenza.
Amesema Tuzo hiyo imeongeza morali kwa wafanyakazi kwa kuendelea kufanya kazi bora na nzuri katika kutoa huduma kwa umma.
"Tunashukuru uongozi kwani unatuwezesha kwa yale yote tunayoyataka ili kurahisisha huduma bora kwa wateja wetu",Amesema.
Sambamba na hayo Lupenza amesema kupitia huduma ya Jisoti ambayo inatolewa na shirika hilo inamsaidia mwananchi kuweza kupata huduma zote na kuripoti changamoto yeyote ya umeme pindi inapojitokeza.
"Sasa hivi tunekuja na huduma ya Jisoti ili kumsaidia mteja kupata huduma zetu na kuripoti changamoto ya umeme kwa kutumia simu yake ya mkononi kwa kutumia namba 0748550000",Amesema.
Aidha ametoa rai kwa wananchi kutembelea banda lao lililopo ndani ya viwanja vya maonesho saba saba ili waweze kupata elimu kuhusu miradi mbalimbali inayotekelezwa na shirika ukiwemo mradi mkubwa wa bwawa la Mwalimu Nyerere.
0 Comments