Na, Mwandishi Wetu – DODOMA
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Ridhiwani Jakaya Kikwete amehimiza menejimenti na watumishi wa ofisi hiyo kuongeza ufanisi katika kuratibu shughuli za vijana na masuala ya ajira nchini ili kutimiza matarajio ya vijana katika kukuza maendeleo ya Taifa.
Aidha, Mhe. Ridhiwani amesema kuwa dhamira ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuona vijana ambao ndio nguvu kazi ya taifa wanapata ajira zinazozalishwa na sekta mbalimbali nchini.
Amesema hayo leo Julai 31, 2024 wakati alipowasili kwenye hiyo Ofisi iliyopo Mji wa serikali Mtumba kwa mara ya kwanza baada ya kuapishwa Ikulu, Jijini Dar es Salaam tarehe 26 Julai, 2024.
Vile vile Mhe. Ridhiwani Kikwete amesema, Wananchi ambao kwa asilimia kubwa ni vijana wanatarajia makubwa kupitia wizara hiyo ambayo inasimamia maeneo mbalimbali ikiwemo masuala ya maendeleo ya Vijana, Ajira, ustawi wa Watu wenye Ulemavu, Wafanyakazi, Waajiri na Wastaafu.
“Matarajio yangu ni kuona tunawafikia vijana kwa wingi, kutambua changamoto zanazowakabili na kutatua changamoto hizo,” amesema Mhe. Ridhiwani
Kwa upande mwengine, Mhe. Ridhiwani Kikwete amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumteua kuwa Waziri katika Ofisi hiyo na kuahidi kushirikiana na watumishi wa Ofisi yake ili kufanikisha malengo na mipango yaliyokusudiwa na Serikali katika kuwahudumia wananchi.
Waziri Ridhiwani Kikwete amewasili katika ofisi hiyo ambapo alipokelewa na Katibu Mkuu, Mhe. Mary Ngelela Maganga.
0 Comments