Na Grace Semfuko- MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali inatambua mchango wa taasisi ya Mkapa Foundation katika sekta ya afya na kwamba imekuwa ikisaidia kwa kusomesha watumishi wengi katika sekta ya hiyo ambao wanatoa huduma katika maeneo mbalimbali nchini.
Rais Samia ameyasema hayo leo Julai 31 jijini Dar es Salaam wakati akihutubia mkutano wa tatu wa kumbukizi za Rais wa Awamu ya Tatu, Hayati Benjamin William Mkapa.
"Serikali inaridhika sana na inatambua mchango mkubwa unaotolewa na taasisi hii ya Benjamin Mkapa Foundation, ndani ya miaka 18 taasisi imesomesha watumishi wa afya watarajiwa na watumishi walioko kazini takribani 1100 katika fani mbalimbali zikiwemo za matibabu, wauguzi wakunga na wengine," ameeleza Rais Samia.
Pamoja na hilo, Rais Samia amesema Hayati Mkapa anakumbukwa kama baba wa mifumo, baba wa taasisi na baba wa mageuzi.
“Urithi aliotuachia Hayati Rais Benjamin Mkapa, unamfanya aendelee kuishi hata baada ya kifo chake. Mzee Mkapa anakumbukwa kama Baba wa taasisi, Baba wa mifumo na Baba wa mageuzi," ameeleza Rais Samia.
Kwa upande wake Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Bw. Thobias Makoba amesema Hayati Mkapa ndiye aliyeasisi mradi wa treni ya mwendo kasi inayotumia reli ya kisasa (SGR), kwa kutoa wazo ambalo utekelezaji wake katika kipande cha Dar es Salaam hadi Dodoma umekamilishwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Mkapa anaendelea kumbukwa kwa kuasisi Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ambao unatekeleza miradi ya kuzikomboa kaya masikini kwa kuwapa misaada ya kifedha, maarifa ya biashara, na misaada mbalimbali yenye umuhimu sana katika ustawi.
Pamoja na hayo, Mkapa ataendelea kumbukwa nchini Tanzania kama muasisi wa taasisi nyingi za kiutendaji ikiwamo Mamlaka ya Kodi Tanzania (TRA) yenye wajibu wa kukusanya mapato ambayo yanatumika katika kuitekeleza miradi ya maendeleo inayotoa huduma kwa jamii.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akihutubia viongozi mbalimbali wakati wa kilele cha Kumbukizi ya 3 ya Urithi wa Mkapa katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam tarehe 31 Julai, 2024.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa na Rais wa Zanzibar Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi ambaye pia ni Msarifu wa Taasisi ya Benjamin Mkapa wakati walipotembelea mabanda ya Maonesho ya wadau wa Taasisi hiyo katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam tarehe 31 Julai, 2024.
Viongozi mbalimbali waliohudhuria Kumbukizi ya 3 ya Urithi wa Mkapa katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam tarehe 31 Julai, 2024.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa pamoja na viongozi mbalimbali wakati wa kilele cha Kumbukizi ya 3 ya Urithi wa Mkapa katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam tarehe 31 Julai, 2024.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akitoa Tuzo ya Mkapa kuhusu Uongozi thabiti kwa Washindi mbalimbali kutoka Sekta ya Afya Nchini.. Mhe. Rais Samia alitoa Tuzo hizo wakati wa kilele cha Kumbukizi ya 3 ya Urithi wa Mkapa katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam tarehe 31 Julai, 2024.
0 Comments