Ticker

6/recent/ticker-posts

NEMC YATAKIWA KUTOAJI USHAURI WA KIUFUNDI KWENYE MAOMBI YA VYETI VYA TATHIMINI YA MAZINGIRA

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Ashatu Kijaji amelielekeza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuongeza kasi ya utoaji wa vyeti vya tathimini ya mazingira katika miradi inayotekelezwa nchini.

Dkt. Kijaji amesema hayo Julai 11, 2024 Jijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake ya kutembelea Ofisi za NEMC kwa ajili ya kuzungumza na Menejimenti pamoja na kufahamu majukumu ya kisheria yanayosimamia Baraza hilo.

Amesema katika kipindi hiki, Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kujipambanua katika kufungua milango kwa wawekezaji wa miradi ya maendeleo nchini, juhudi ambazo zinahitaji kuungwa mkono kwa vitendo na taasisi zote za umma ikiwemo NEMC.

“Natambua mmeendelea kufanya kazi nzuri katika kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Mazingira Sura 191…Naomba hili la vyeti vya tathimini ya mazingira tuliangalia kwa jicho la kipekee ili kuwezesha utekelezaji wa miradi” amesema Dkt. Kijaji.

Aidha Waziri Kijaji amefafanua kuwa Ofisi yake ina imani na matumaini makubwa na watendaji wa Baraza hilo katika kuakisi maono ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika usimamizi na uhifadhi endelevu wa mazingira ili kulinda afya na maisha ya Watanzania.

Ameeleza kuwa NEMC inapaswa kuwa kiungo katika kutoa ushauri wa kiufundi na kitaalamu wakati wa mchakato wa maombi ya vyeti vya tathimini ya mazingira kwa kuhakikisha waombaji wanapatiwa maelekezo ya namna bora ya kushughulikia kasoro na changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika maeneo ya miradi.

“Tunapobaini kasoro au changamoto wakati wa maombi ya vyeti tutoe msaada wa haraka ili waombaji waweze kuzirekebisha na kutoa taarifa na kuwajulisha mapema na pia tusichukue muda mrefu kwa waombaji wakisubiri huduma hii” amesema Dkt. Kijaji.

Akifafanua zaidi Dkt. Kijaji amesema Watanzania wana imani na matumaini makubwa na Baraza hilo katika usimamizi endelevu wa mazingira na hivyo kuiwezesha Tanzania kuwa na jamii salama kwa mustakabali wa vizazi vya sasa na vijavyo.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Khamis Hamza Khamis amesema Serikali itaendelea kujenga mazingira wezeshi kwa Baraza hilo ikiwemo kusimamia mchakato wa mabadiliko ya muundo wa Baraza hilo ambao upo katika hatua nzuri.

Ameongeza kuwa Baraza hilo lina wataalamu wenye ujuzi, weledi na maarifa ya kitaaluma katika usimamizi na uhifadhi wa mazingira, hivyo utaalamu huo hauna budi kutumika vyema katika kubuni na kubaini miradi inayoweza kutoa suluhisho ya changamoto za uharibifu wa mazingira nchini.

“NEMC ina wasomi wazuri wenye fani mbalimbali ambao wakitumika vyema wataisaidia nchi kuweza kupiga hatua kubwa na pia kuandaa mipango itakayosaidia kupata majibu ya changamoto za uharibifu wa mazingira katika taifa letu” amesema Mhe. Khamis.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NEMC, Prof. Esnati Chaggu ameishukuru Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kuendelea kuiwezesha Bodi kutekeleza vyema majukumu yake kupitia Mpango Kazi ulioandaliwa na menejimenti ya baraza hilo.

Amesema katika kuharakisha kasi ya utekelezaji wa majukumu, baraza limebuni mfumo ya kieletroniki kupitia TEHAMA ambapo huduma mbalimbali zinazotolewa katika mfumo huo ikiwemo vyeti vya tathimini ya mazingira na hivyo kurahisisha utendaji kazi.

Kuhusu usimamizi wa Sheria, Prof. Chaggu amesema baraza limeendelea kusimamia utekelezaji wa sheria ya upigaji marufuku wa matumizi ya mifuko ya plastiki kwa kushirikiana na mamlaka mbalimbali za Serikali na sekta binafsi.

“Tunaishukuru Serikali kwa ushirikiano unaoipatia baraza..tunaahidi kuongeza kasi, weledi na maarifa zaidi katika kufanikisha utekelezaji wa majukumu ili tuweze kuleta tija iliyokusudiwa kwa kuzingatia maono ya Viongozi wetu” amesema Prof. Chaggu.

Aidha kwa upande Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Immaculate Sware amesema Baraza litaendelea kupokea na kutekeleza maelezo yanatolewa na Viongozi Wakuu wa Serikali katika kusimamia Sheria ya Mazingira Sura 191.

“Baraza limeendelea kufanya kazi kubwa…Tupo tayari kwa kazi na tutauwepo majini na ardhini kwani tuna wataalamu wenye weledi katika kutekeleza majukumu tuliyopewa” amesema Dkt. Sware.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akizungumza jambo wakati wa ziara yake aliyoifanya katika Ofisi za Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Jijini Dar es Salaam Julai 11, 2024. Kulia ni Naibu Waziri wa Ofisi hiyo, Mhe. Khamis Hamza Khamis na Kaimu Katibu Mkuu, Bw. Abdallah Hassan Mitawi
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akizungumza jambo wakati wa ziara ya Mhe. Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Ashatu Kijaji (katikati) katika ofisi za Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Jijini Dar es Salaam Julai 11, 2024. Kushoto ni Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Bw. Abdallah Hassan Mitawi.
Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Bw. Abdallah Hassan Mitawi akizungumza jambo wakati wa ziara ya Mhe. Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Ashatu Kijaji (katikati) katika ofisi za Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Jijini Dar es Salaam Julai 11, 2024. Kulia ni Naibu Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhe. Khamis Hamza Khamis.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Prof. Esnat Chaggu akizungumza jambo wakati wa ziara ya Mhe. Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Ashatu Kijaji (katikati) katika ofisi za Baraza hilo Jijini Dar es Salaam Julai 11, 2024. Kulia ni Naibu Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhe. Khamis Hamza Khamis.
Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. Immaculate Sware akimkakaribisha katika Ofisi za Baraza hilo, Mhe. Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Ashatu Kijaji (mbele) wakati wa ziara yake aliyoifanya katika Baraza hilo Jijini Dar es Salaam Julai 11, 2024.
Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. Immaculate Sware (katikati) akimkakaribisha katika Ofisi za Baraza hilo, Mhe. Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Ashatu Kijaji (mbele) wakati wa ziara yake aliyoifanya katika Baraza hilo Jijini Dar es Salaam Julai 11, 2024.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Ashatu Kijaji akiwa pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Prof. Esnat Chaggu na Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Immaculate Sware wakifuatilia Makala mjongeo kuhusu majukumu ya Baraza hilo wakati wa ziara yake aliyoifanya katika Baraza hilo Julai 11, 2024 Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Ashatu Kijaji (kulia) akiwa na Naibu Waziri wake, Mhe. Khamis Hamza Khamis wakifuatilia makala mjongeo kuhusu majukumu ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira wakati wa ziara yake aliyoifanya katika Baraza hilo Julai 11, 2024 Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais, Bi. Kemilembe Mutasa akijitambulisha kwa Mhe. Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji wakati wa ziara ya Mhe. Waziri katika Ofisi za Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Jijini Dar es Salaam Julai 11, 2024. Katikati ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Sarah Kibonde.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akisalimiana na Naibu Waziri wa Ofisi hiyo, Mhe. Khamis Hamza Khamis (katikati) muda mfupi baada ya kuwasili katika Ofisi za Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya ziara ya kikazi. Kushoto ni Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Bw. Abdallah Hassan Mitawi.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Ashatu Kijaji akiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. Immaculate Sware kuwasili katika Ofisi za Baraza hilo Jijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake ya kikazi Julai 11, 2024.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Ashatu Kijaji akisaini kitabu cha wageni muda mfupi baada ya kuwasili katika Ofisi za Baraza hilo Jijini Dar es Salaam Julai 11, 2024 kwa ajili ya ziara ya kikazi.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis (wa pili kushoto), Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Bw. Abdallah Hassan Mitawi na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira Prof. Esnat Chaggu wakibadilishana mawazo muda mfupi kabla ya kuwasili kwa Mhe. Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Ashatu Kijaji katika Ofisi za NEMC Jijini Dar es Salaam Julai 11, 2024.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Ashatu Kijaji akiwa (katikati), Naibu Waziri wa Ofisi hiyo, Mhe. Khamis Hamza Khamis (kushoto) na Kaimu Katibu Mkuu, Bw. Abdallah Mitawi (kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi na watendaji wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Jijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake aliyoifanya katika Ofisi hiyo Julai 11, 2024.

Post a Comment

0 Comments