Ticker

6/recent/ticker-posts

NAIBU WAZIRI KHAMIS AITAKA NEMC KUONDOA VIKWAZO KWENYE HIFADHI HAI YA RUMAKI

NA EMMANUEL MBATILO

BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazinrira (NEMC) limetakiwa kuondoa vikwazo vyote vilivyopo katika Hifadhi hai ya RUMAKI hasa suala la kuangalia ongezeko la idadi ya watu ndani ya eneo la Hifadhi.

Wito huo umetolewa leo Julai 19, 2024 mkoani Pwani na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis wakati wa uzinduzi na ufunguzi wa Hifadhi Hai ya RUMAKI ambapo wadau mbalimbali wameweza kushiriki katika tukio hilo.

Aidha Naibu Waziri amewataka NEMC kuweka na kutumia mfumo maalum wa tahadhari na kuwa na ufuatiliaji wa mara kwa mara kupunguza changamoto za mioto, uchafuzi wa mazingira, ukataji misitu ikiwemo mikoko na uvuvi haramu.

Pamoja na hayo Naibu Waziri amewaelekeza NEMC kuendelea kuelimisha na kuhamasisha jamii juu ya umuhimu wa kulinda na kutunza hifadhi hiyo kwa faida endelevu ya eneo la RUMAKI na nchi kwa ujumla.

Tukiyafanya haya na mengine, kutaisaidia Hifadhi hii kuendelea kubaki kwenye ubora wake na haswa kwa kuwa Hifadhi Hai Dunia hufanyiwa tathmini kila baada ya miaka 10 na kutoa ripoti ambayo inawasilishwa UNESCO" amesema

Amesema kuwa tunapaswa kuhakikisha Hifadhi Hai hiyo inabaki kuwa kwenye ubora na viwango vinavyokubalika kwa mujibu wa vigezo vyetu vya ndani na vya UNESCO kwani kutasaidia Hifadhi hiyo kuendelea kuwa na umuhimu wa kijamii, kiuchumi, kitalii na kimazingira na hivyo, itabaki kuwemo kwenye mtandao wa Hifadhi Hai Duniani.

Hata hivyo ameeleza kuwa mifumo ikolojia iliyopo katika Hifadhi Hai ni miongoni mwa bioanuai muhimu za Ukanda wa Pwani ya Afrika Mashariki inayohifadhi bioanuai nyingi na za kipekee zinazotambulika kitaifa na kimataifa.

Amesema kuwa pamoja na RUMAKI kuwemo kwenye Hifadhi Hai inayotambuliwa na UNESCO, bado Msitu wa mikoko na misitu ya asili iliyoko Rufiji na Kibiti, malikale ya Kilwa, Hifadhi ya Maeneo tengefu ya Bahari ya Mafia, utabaki kuwa katika hali ya uangalizi chini ya sheria husika za nchi yetu kupitia Taasisi zilizokasimiwa majukumu hayo.

Kwa Upande wake,Mkurugenzi wa Tafiti za Mazingira NEMC Dkt. Menan Jangu akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu NEMC amesema ni muhimu kuyatambua maeneo ya nchi ambayo yanasifa ya kuingia katika kumbukumbu za kidunia kwani yatachochea maendeleo endelevu pamoja na uhifadhi.

Pamoja na hayo Dkt. Jangu amesema ushirikishwaji kwa wananchi pamoja na kulinda maeneo hayo ya Hifadhi Hai itasaidia kuendelea kutunza sifa za maeneo hayo.

Nae,Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkazi WWF Tanzania Bi. Joan Itanisa ameahidi kuwa wataendelea kushirikiana na serikali pamoja na wananchi wanaozunguka Hifadhi ya RUMAKI, kwa lengo la kuhakikisha rasilimali zinazopatikana katika hifadhi hiyo zinaendelea kulindwa ili kukuza utalii nchini ili kuboresha hali ya maisha ya wananchi na kuingizia taifa kipato.

Vilevile, Afisa Programu wa Tume ya Taifa ya UNESCO, Bw. Noel Musanze Yocta amewashukuru wadau walioshiriki katika upatikanaji wa hifadhi sita nchini ambazo miongoni ni Ngorongoro,Serengeti,lake manyara,zilizopatikana kutokana na kamati ya kitaifa ya hifadhi Hai inayo ongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa NEMC.

"Tume ya Taifa ya UNESCO itashirikiana na NEMC pamoja na wadau wengine nchini ili kuunga Juhudi za kamati hii,ya kugundua maeneo mengi zaidi na kyaiingiza katika mtandao wa Hifadhi duniani kwa mujibu wa taratibu za UNESCO" Amesema.

Post a Comment

0 Comments