Ticker

6/recent/ticker-posts

DKT. HASHIL AZINDUA SHEREHE ZA MIAKA 60 YA CBE

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah amekipongeza Chuo Cha Elimu ya Biashara (CBE) kwa mafanikio yake ndani ya miaka 60 na kusisitiza umuhimu wa Chuo hicho katika kutoa elimu bora ya biashara na kuandaa wataalamu wenye ujuzi.

Pongezi hizo amezitoa leo Julai 3, 2024 wakati akizindua Sherehe za miaka 60 ya Chuo hicho katika Kampasi Kuu ya CBE Jijini Dar es Salaam ambapo viongozi mbalimbali pamoja na wanafunzi wameshiriki kwenye hafla hiyo.

Aidha Dkt. Hashil ameipongeza dira ya "CBE Visoin 2074" inayolenga maendeleo ya teknolojia, utandawazi, na mabadiliko ya kijamii na kiuchumi na vilevile amesisitiza umuhimu wa taasisi za elimu kubuni mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya teknolojia.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Uongozi wa Chuo, Prof. Wineaster Anderson ameeleza kuwa CBE imepiga hatua kubwa katika kutoa elimu ya biashara, kufanya tafiti na kutoa ushauri wa kitaalamu tangu kuanzishwa kwake kwa sheria ya Bunge Namba 31 ya mwaka 1965.

Amebainisha kuwa Chuo kimepanua wigo wake kwa kufungua kampasi Dodoma, Mwanza na Mbeya, na pia amesisitiza umuhimu wa sera na mikakati mbalimbali zilizoboresha utendaji wa kitaasisi, ikiwa ni pamoja na sera za Afya na Usalama wa Wafanyakazi, Uhasibu na Makadirio, Usalama wa ICT, na Usimamizi wa Mali.

Pamoja na hayo Prof. Anderson amesema CBE imeimarisha miundombinu, rasilimali watu na uwezo wa kifedha. "Chuo kimeanzisha miradi ya uwekezaji kwa ushirikisho na sekta binafsi ili kuongeza mapato na kuimarisha maendeleo ya kitaaluma na miundombinu" amesema Prof. Anderson.

Nae Mkuu wa Chuo, Prof. Edda Lwoga ameelezea historia na mafanikio ya CBE tangu kuanzishwa kwake mwaka 1965 na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Amesema CBE inajivunia kuwa na Kampasi nne nchini na kutoa elimu bora kwa wanafunzi zaidi ya 19,000.

Hata hivyo amebainisha kuwa CBE imepanua programu zake hadi zaidi ya 22 mwaka 2024, ikijumuisha Biashara, Uhasibu, Masoko, Manunuzi na Ugavi, TEHAMA na nyinginezo.

Pia ametambulisha dira ya miaka 50 ya CBE, "CBE Vision 2074, " inayolenga maendeleo endelevu kupitia teknolojia mpya na tafiti za kina.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah akikata upete kuashiria uzinduzi wa Miaka 60 ya  Sherehe za miaka 60 ya Chuo hicho katika Kampasi Kuu ya CBE Jijini Dar es Salaam uliofanyika leo Julai 3, 2024 Jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah akikata upete kuashiria uzinduzi wa Miaka 60 ya  Sherehe za miaka 60 ya Chuo hicho katika Kampasi Kuu ya CBE Jijini Dar es Salaam uliofanyika leo Julai 3, 2024 Jijini Dar es Salaam.

Post a Comment

0 Comments