Ticker

6/recent/ticker-posts

DCEA YAMSHIKILIA MTUHUMIWA WA DAWA ZENYE ASILI YA KULEVYA TAKRIBANI LITA 16,523

MAMLAKA Ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA,) inamshikilia Shaban Musa Adam (54,) mkazi wa Dar es Salaam kwa tuhuma za kutengeneza dawa za kulevya ambapo pia amekamatwa na  kemikali bashirifu na dawa tiba zenye asili ya kulevya takribani lita 16,523 ambazo zimekwisha muda wa matumizi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Kamishina Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA,) Aretas Lyimo amesema Juni 11, 2024 mtuhumiwa huyo alikamatwa nyumbani kwake Manzese Kilimani jijini Dar es Salaam akitengeneza dawa za kulevya alizozitambulisha kama Heroin kwa kutumia dawa tiba zenye asili ya kulevya akichanganya kemikali bashirifu.

"Dawa hizi zinaweza kusababisha madhara makubwa kiafya kwa mtumiaji kama vile magonjwa ya moyo, ini, Figo, mfumo wa hewa, saratani, magonjwa ya akili pamoja na uraibu." Amesema.

Amesema, Baada ya kutengeneza dawa hizo mtuhumiwa huyo husafirisha kwa kutumia mabasi ya abiria kama vifurushi kwenda katika mikoa mbalimbali hususani katika miji mikubwa nchini.

" Mtuhumiwa huyo ameieleza Mamlaka kuwa, siku za nyuma alikuwa akitengeneza dawa hizo za kulevya katika Nchi za bara la Asia kwenye magenge ya wazalishaji wa dawa za kulevya na pia alitumika kama mbebaji wa dawa hizo maarufu kama punda na aliporejea nchini aliendelea na uhalifu huo."Amesema.

Katika hatua nyingine Mamlaka hiyo inamshikilia mtu mmoja mtanzania aliyetambulika kwa jina la Mbaba Rabin Issa mwenye hati ya kusafiria (Passport,) TAE442718 ambaye alikamatwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Melchior Ndadaye Bujumbura, Burundi akiwa na kilogramu 3.8 za Skanka, Dawa zilifichwa kwa kushonewa ndani ya begi la nguo na mtuhumiwa huyo alikamatwa akijiandaa kusafiri kuelekea Dubai.

"Kufuatia mikataba ya kikanda na kimataifa ambayo Tanzania imesaini katika Udhibiti wa Dawa za Kulevya, Mhalifu yeyote wa dawa za kulevya atakayefanya uhalifu katika Nchi zilizoingia makubaliano na kukimbilia kwenye moja ya Nchi hizo atakamatwa." Amesema.

Aidha amesema kuwa Mamlaka hiyo imekamilisha kanzi data ya wauzaji wakubwa wa dawa za kulevya na imeanza uchunguzi juu ya watu hao.

"Wengi wamebainika wapo ndani ya Nchi na wengine nje ya Nchi... Baadhi yao wanajihusisha na biashara nyingine halali lakini wanajihusisha na biashara ya dawa za kulevya na kufanya utakatishaji, Mamlaka inatoa wito kwao kuachana mara moja na biashara hiyo na kujikita na biashara halali kwa kuwa uchunguzi dhidi yao unaendelea na hatua kali za kisheria zitachukuliwa." Amefafanua.

Vilevile amesema kupitia Ofisi za Kanda za Mamlaka hiyo zimefanyika Operesheni katika mikoa ya Dodoma, Mwanza, Mtwara na Mbeya gunia 285 za bangi kavu, kilogramu 350 za aina mbalimbali za dawa za kulevya, milimita 115 za dawa tiba zenye asili ya kulevya pamoja na lita 16,523 za kemikali bashirifu zilizokuwa zinasambazwa kinyume na sheria vilikamatwa pamoja na watuhumiwa 48.

Akieleza madhara ya matumizi ya dawa za kulevya Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Mohamed Janabi amesema, katika Kanzi data ya hospitali hiyo mpaka Juni mwaka watu 3840 wanatumia Methadone na kila siku watu 900 wanakunywa dawa tiba ya Methadone na kuwa kituo chenye watu wengi zaidi waliothirika na dawa za kulevya hapa nchini

Amesema, Kiafya dawa zote zinazotumika hapa nchini lazima zipimwe na TMDA na kuainishwa faida yake na kueleza kuwa matumizi ya dawa za kulevya huingiliana na mfumo wa umeme wa moyo kusababisha a vifo vya ghafla, matatizo ya Figo, saratani ya ini na afya ya akili.

" Tunawashauri hata wale wanaotumia Methadone wasichanganye na hizi dawa za kulevya kwa kuwa matokeo yake sio mazuri." Ameeleza.

Katika mkutano huo pia uliambatana na zoezi la utoaji wa tuzo za kutambua mchango wa taasisi za Serikali na zisizo za Kiserikali ikiwemo Hospitali ya Taifa Muhimbili, Kituo cha utangazaji cha ITV, TMDA, Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Taasisi ya Pili Misana na Ofisi ya RPC Mkoa wa Tanga ambazo zimekuwa mstari wa mbele katika kupiga vita dawa za kulevya.

Post a Comment

0 Comments