Na Mwandishi Wetu, Tanga
WAENDESHA bodaboda waliopo eneo la Kabuku wilayani Handeni mkoani Tanga wameliomba shirika la Amend Tanzania kupitia ufadhili wa Ubalozi wa Uswisi nchini kuendelea kuwapatia mafunzo ya usalama barabara ili kupunguza ajali za barabarani.
Wakizungumza baada ya kupatiwa mafunzo ya usalama barabarani yaliyokwenda sambamba na mafunzo ya utoaji huduma ya kwanza iwapo ajali imetokea, waendesha bodaboda hao wamesema mafunzo ambayo wameyapata yamewezesha kutambua vema sheria za usalama barabarani hivyo watakuwa makini.
“Kuna waendesha pikipiki wachache ambao angalau wanajua sheria za usalama barabarani lakini wengi wao wanaendesha kwa mazoea, hawajui sheria na hata kama wanazifahamu basi hakuna anayezifuata na matokeo yake ajali za barabarani zinazohusisha bodaboda zimekuwa nyingi.
“Hivyo kupitia mafunzo haya ambayo tumeyapata kutoka kwa Amend Tanzania na Jeshi la Polisi tunaamini kuanzia sasa tutakuwa makini barabarani kwani tayari tumepata elimu na kuelezwa sheria mbalimbali zinazohusu usalama barabarani,”amesema dereva bodaboda Shaban Mhando.
Kwa upande wake Mratibu wa Amend Tanzania Ramadhan Nyanza amesema mafunzo ya usalama barabarani ambayo yametolewa kwa maofisa usafirishaji hao (bodaboda) ni mwendelezo wa kampeni ya kuhakikisha vijana hususan waendesha bodaboda wanakuwa salama wawapo barabarani.
Amesisitiza katika mafunzo hayo zaidi ya waendesha bodaboda 160 wa Wilaya ya Handeni wamepatiwa mafunzo na kufafanua kuwa changamoto kubwa ni waendesha bodaboda wengi kutofuata sheria za usalama barabarani na hivyo kusababisha ajali zinazokatisha maisha au kusababisha ulemavu wa kudumu.
Hivyo Shirika la Amend Tanzania kupitia ufadhi wa Ubalozi wa Uswis nchini wameona iko haja ya kutoa mafunzo hayo kwa lengo la kupunguza ajali za barabarani au kuzimaliza kabisa.
“Mafunzo haya yamefanyika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Tanga na sasa tumefika Handeni kutoa mafunzo kwa waendesha bodaboda ambao wamekumbushwa umuhimu wa kufuata sheria na alama za barabarani pamoja na kupatiwa mafunzo ya kutoa huduma ya kwanza,” amesema.
Awali Kaimu Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Wilaya ya Handeni Inspekta Gwantwa Mwakisole, amesema changamoto kubwa wanayoipata waendesha pikipiki katika barabara kubwa (kuu) za kuunganisha mikoa ni wingi wa magari yanayopita kwa kasi kubwa, hivyo kusababisha ajali nyingi.
“Asilimia kubwa ya waendesha pikipiki hawajapitia mafunzo na hawatambui matumizi salama ya barabara hadi kusababisha ajali kwa kusababisha wao wenyewe au kusababishiwa,” amesema.
Ameongeza kuwa, kampeni hiyo inayoratibiwa na Amend kwa ufadhili wa ubalozi wa Uswiss nchini kufika wilayani Handeni eneo la Kabuku wanashukuru kufikiwa na mafunzo hayo.
“Tunaomba nafasi zijazo za mafunzo waje kuweka kambi katika eneo letu la Handeni, tutawapa ushirikiano mzuri kwani katika mafunzo ambayo wanamepata waendesha pikipiki unaona kabisa tunakwenda kupunguza ajali za barabarani hapa kwetu,” amesema.
0 Comments