Ticker

6/recent/ticker-posts

BODABODA KOROGWE WAKUMBUSHWA KUFUATA SHERIA ,KUWA NA BIMA, LESENI

Na Mwandishi Wetu,Tanga

WAENDESHA bodoboda katika Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga wapatiwa mafunzo ya elimu ya usalama barabarani kwa lengo wa kuwakumbusha umuhimu wa kufuata Sheria ili kuepuka ajali zinazosababisha vifo na ulemavu wa kudumu kwa baadhi yao.

Mafunzo hayo ya elimu ya Usalama Barabarani yanatolewa na Shirika la Amend Tanzania kwa ushirikiana na wadau muhimu kama Jeshi la Polisi Kikosi cha usalama Barabarani na Mafunzo yamefadhiliwa na Ubalozi wa Uswiss nchini.

Akizungumza wakati wa Mafunzo hayo kwa waendesha bodaboda wa Wilaya ya Korogwe Koplo Hamisi Mbilikila kutoka Ofisi ya Mkuu wa Usalama Barabarani Mkoa wa Tanga amesema Kuna kila sababu ya waendesha bodaboda hao kupata elimu itakayowezesha kufahamu Sheria na kuzifuata ili wawe salama.

"Wenzetu wa Amend kwa ufadhili wa Ubalozi wa Uswiss wameguswa na ajali zinazotokea kwa waendesha pikipiki nchini, ,wameangalia takwimu na kubaini waendesha pikipiki ndio watu ambao wanapoteza maisha pamoja na kupata ulemavu.

"Sasa kwasababu ya hilo wameona waje wilayani Korogwe kwa kuwa kuna umuhimu wa elimu ya usalama barabarani itakayotolewa na Shirika la Amend kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi.Hapa Korogwe ni Wilaya ambayo kwa Mkoa Wetu wa Tanga inaongoza kwa ajali za barabarani kwasababu kuna barabara kuu,"amesema.

Amefafanua katika Wilaya hiyo pia Kuna bodaboda na bajaji nyingi ukilinganisha na Wilaya nyingine za mkoa huo , hivyo ni Wilaya ambayo wanaiangalia kwa hicho la karibu huku akisisitiza wanatoa elimu kwa waendesha bodaboda kwa kutambua riziki zao zinategemea vyombo vya moto.

"Tunataka mjifunze sana kuhusu elimu ya usalama barabarani kwasababu riziki zenu mnazipata kwa kutumia vyombo vya moto hivyo mnapaswa kuviheshimu vyombo hivyo pamoja na sheria za usalama barabarani Ukienda kinyume tu utakuta hela yote inaishia katika faini za barabarani kwasababu tu ya kutofuata Sheria,"amesema

Amewakumbusha kuvaa kofia ngumu kwasababu ajali nyingi zinazotokea kichwa ndio hupata madhara makubwa ,hivyo ni muhimu kuvaa kofia hiyo ili kujikinga na madhara yanayoweza kutokea baada ya ajali.

"Tunatoa elimu ya Mafunzo ya usalama barabarani ili msife ,wote tunafahamu tunaowajibu wa kushirikiana kukomesha ajali na sisi Jeshi la Polisi tunaowajibu wa kuhakikisha tunasimamia sheria za barabarani ili watumiaji wa vyombo vya moto wawe salama."

Pia amesema sheria inataka mwendesha bodaboda kuvaa kofia ngumu, kuwa na leseni ya udereva,kuwa na bima pamoja na kutobeba abiria zaidi ya mmoja,hivyo ni vema wakazingatia Sheria hizo kuepuka faini lakini na kwa usalama wao na vyombo vyao.

Akielezea zaidi amesema pikipiki ni usafiri wa haraka lakini umesaidia watu wengi kupata riziki kwa kutumia bodaboda na ndio maana hata watu wanafanya kazi nyingine wanapomaliza wanakwenda katika vijiwe kwa ajili ya kubeba abiria wapate riziki.

"Kuna watumishi wakimaliza shughuli zao wanakwenda katika vijiwe kupata vya bodaboda.Hata hivyo baadhi ya bodaboda wamesababisha muwe mnasemwa ndio maana tumekuja kutoa elimu.Kuna wale wanakwenda spidi amevaa ndala za dada ake na amekalia kalio moja wakataeni hao,ndio wanawaharibia.

Kwa upande wake Mratibu wa Shirika la Amend Ramadhan Nyanza amesema kwa ufadhili wa Ubalozi wa Uswiss wameona ni vema kutoa Mafunzo hayo kwa waendesha bodaboda na hasa kuwakumbusha Sheria za Usalama Barabarani ambazo wakizifahamu na kuzifuata wataepuka ajali.

"Tumeona ni vema tukalifikia kundi hili la bodaboda kwani ni kundi ambalo mbali ya kurahisisha usafiri limekuwa chanzo kikubwa cha ajali za barabarani na tunafahamu wenzetu wa Kikosi Cha usalama barabarani wakisema wafanye operesheni maalum ya bodaboda watakaobakia barabarani zitakuwa bodaboda chache sana,hivyo mafunzo haya tunakuja kuwakumbusha umuhimu wa sheria za barabarani."

Amefafanua kuwa mafunzo hayo ni ya msasa tu kwasababu tayari bodaboda hao ni madereva tayari, hivyo wanachofundishwa ni sheria za Usalama Barabarani pamoja na Mafunzo ya Huduma ya kwanza ili inapotokea ajali waweze kusaidia kuokoa maisha ya mtu ambaye atakuwa amepata ajali.

"Hatufundishi pikipiki inaendeshwaje bali tunatoa elimu ya wewe kuwa salama,jinsi gani unatakiwa kubeba abiria, kwanini tunakwambia usipakie abiria zaidi ya mmoja, jinsi gani unatakiwa kupita magari barabara."


Post a Comment

0 Comments