Ticker

6/recent/ticker-posts

ASASI ZA KIRAIA ZAASWA KUWA MAKINI NA MISAADA KUTOKA NJE


Na Hamida Kamchalla, TANGA.

ASASI zisizo za Kiserikali nchini zimeaswa kujiepusha kupokea fedha za misaada ambazo zinatolewa kwa malengo ambayo ni kinyume na kazi zao na mabadiliko ya Kitaifa katika kuisaidia jamii ikiwa ni pamoja na kupinga vitendo viovu kama ndoa ya jinsia moja.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Balozi, Dkt. Batilda Buriani ameyasema hayo kwenye mafunzo ya Nafasi Asasi za Kiraia (AZAKI) na Asasi zisizo za Kiserikali (AZISE) katika mapambano dhidi ya rushwa kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani 2025.

Dkt. Buriani pia ameziomba Asasi hizo kusaidia siyo tu kupambana na rushwa tu bali katika nyanja mbalimbali ikiwemo upingaji wa ukiukwaji wa haki za binadamu hasa katika kuelekea kipindi hiki cha uchaguzi.

"Tafiti zinaonesha kwamba kuna baadhi ya Asasi zisizo za Kiserikali zilinyooshewa kidole kana kwamba zilijihusisha kwa namna moja au nyingine katika uvunjifu wa maadili na na kusaidia katika vitendo vinavyoenda kinyume na mila na desturi zetu za dini,

"Katika Mkoa wetu wa Tanga, naomba sana sote kwa pamoja tushirikiane kuhakikisha kwamba maswala yanayokwenda kinyume, ikiwemo ndoa ya jinsia moja, tusijihusishe nayo, vitabu vimepatikana huko vinavyo hamasisha ushoga, kabla havijaletwa nchini tujiridhishe kama vinaendana na tamaduni za mila zetu,

"Lakini hata ikiwa msaada wa bidhaa mbalimbali za madawa kama mafuta ya vilainishi, tujiulize ni kwa ajili ya kufanyia kazi gani, tusifanye kazi tu kwakuwa tunataka kupanga bajeti au kuingiza fedha za kigeni kuendesha shukuli zetu za Asasi" amesema.

Naye Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Tanga, Victor Swela amesema lengo kubwa la mafunzo hayo ni kutaka kushirikisha jamii katika mapambano dhidi ya rushwa hasa katika kipindi cha kuelekea uchaguzi.

Swela amefafanua kwamba Asasi zisizo za Kiserikali ziko karibu zaidi na jamii hivyo mafunzo hayo yanakwenda kuelimisha suala la kupambana na rushwa kwa upana zaidi katika ngazi ya jamii lakini pia elimu hiyo itagusa maeneo mbalimbali kwakuwa Bado ni endelevu.

"Tumeshatoa mafunzo kwa vyama vya siasa, jeshi la polisi lakini pia tunaendelea mpaka tuwafikie viongozi wa dini, mafunzo haya kwa Asasi tumetaka kuwakumbusha umuhimu wao katika jamii kule chini na Wana wajibu gani ili kuhakikisha wananchi wanashiriki katika uchaguzi huu bila kushiriki vitendo vya rushwa" amesema.

Amebainisha kwamba kupitia elimu wanayotoa wakipata ushirikiano mzuri kutoka kwa wananchi, wana imani kwamba kama Mkoa watafanikiwa katika kufanya uchaguzi bila vitendo vinavyo sababisha kuwepo kwa rushwa.

"Wananchi watapata elimu kupitia Asasi lakini pia Asasi hizi ndizi zitakazotupatia taarifa kuhusu mienendo ya wagombea au kampeni zinavyoendelea na sisi kuweza kuchukua hatua stahiki kwa atakayebainika kuhusika na vitendo vya rushwa" amesema.

Baadhi ya viongozi wa Asasi hizo wamesema elimu waliyopata itawawezesha kupambana kwa kuwaweka karibu wananchi na kuwapa elimu hiyo ili kuweza kuepuka rushwa katika uchaguzi.

Asasi zipatazo 40 katika Mkoa wa Tanga zimepatiwa mafunzo hayo na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani humo.

Post a Comment

0 Comments