Ticker

6/recent/ticker-posts

ACHENI KUTOZA MGONJWA POSHO YA MUUGUZI NA DEREVA WA GARI LA WAGONJWA - WAZIRI UMMY.


Na Hamida Kamchalla, TANGA.

WAZIRI wa Afya Ummy Mwalimu amepiga marufuku hospitali zote nchini kutoza gharama za muuguzi na dereva wanaomsindikiza mgonjwa kutoka hospitali moja kwenda nyingine katika gari la kubebea wagonjwa (Ambulance) kutoka kwa mwananchi mwenye mgonjwa.

Waziri Mwalimu amepiga marufuku hiyo wakati akikabidhi gari la kubebea wagonjwa katika hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Tanga (Bombo) ikiwa ni moja ya magari ya kubebea wagonjwa 727 yaliyotolewa na serikali kwajili ya kusambazwa katika halmashauri mbalimbali nchini.

Mbali na kupiga marufu hiyo, aliagiza garama hizo ziende moja kwa moja katika hospitali husika ili kumpunguzia mwananchi mzigo mkubwa, huku akitaka mwananchi kuchangia mafuta peke yake.

"Nitoe wito kwa Waganga wakuu wa Mikoa, nchini kote kufanya mapitio ya gharama za wananchi kuchangia huduma za gari ya kubebea wagonjwa ili kuepuka malalamiko kutoka kwa wananchi" amesema.

"Mganga Mkuu wa Mkoa uko hapa na waganga wakuu wa Mikoa yote 26 ya Tanzania bara kila mtu afanye mapitio ya gharama za Ambulance na tukubaliane gharama ambazo ndio husika na kama imetokea kuna wagonjwa wawili wanachangia gharama basi na ile sawa" alisema.

Amebainisha kwamba serikali inanunua magari hayo kwa gharama kubwa hivyo ni jambo la kuumiza kuona ndani ya muda mfupi gari imeanguka na kwamba serikali inapaswa kuhakikisha madereva wake wanazingatia sheria na taratibu za usalama barabarani.

"Tunataka magari ya kubeba wagonjwa yatunzwe yafanyiwe matengenezo ili yaweze kukaa kwa muda mrefu kwasababu serikali inatumia fedha nyingi sana kuyanunua, mfano hii gari ya leo tumetumia shilingi milioni 100 kuinunua,

"Kila Mkoa unapaswa kutenga fedha kwajili ya matuzo na matengenezo ya magari ya haya kwakuwa ni lazima yafanyiwe matengenezo ya mara kwa mara na kila inapobidi" amesisitiza.

Vilevile Waziri Mwalimu amesema serikali kupitia Wizara ya Afya inaendelea kuhakikisha hospitali za Rufani katika Mikoa yote nchini zinakuwa na madaktari bingwa ili mambo mengi yamalizikie kwenye Mikoa badala ya watu kupelekwa mbali zaidi.

Naye Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wq Tanga Dkt. Imani Clemence amesema Ambulance iliyokabidhiwa imetimiza idadi ya Ambulance 15 kwa Mkoa mzima ambapo majimbo 12 yote yamefikiwa na magari hayo.

"Naomba kwa niaba ya Mkoa nikuahidi kwamba tutazitumia gari hizi kama ilivyoelekezwa, tutazitunza, na kuzifuatilia kila zinapokuwa zinafanya safari zake na kuhalikisha zinakuwa salama na kutoa zile zinazostahili" amesema.

Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufani Bombo Dkt. Frank Shega amesema gari hiyo ya wagonjwa itaendelea kuboresha huduma za afya kwenye hospitali hiyo kwani Rufani tunaendelea kuwafikia.

"Nikuhakikishie mheshimiwa Waziri gari hii uliyotukabidhi leo tutaitunza kwa uwezo wetu wote tukiamini jitihada mheshimiwa Rais anazozifanya mpaka tumeweza kupata Ambulance hii zitakwenda kuwahudumia wananchi wetu kwa weledi zaidi" alisema Dkt Shega.

Post a Comment

0 Comments