Ticker

6/recent/ticker-posts

ZAIDI YA SH BILIONI 128 KUTUMIKA MRADI WA SMARTWASOMI, AIRTEL.


Na Hamida Kamchalla, TANGA.

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amezindua mradi wa Airtel SmartWasomi utakaoendeshwa kwa kipindi cha miaka mitano huku zaidi ya sh Bilioni 128,262 zikitarajiwa kutumika ambazo ni sawa na dola za Marekani USD 50,299,062.

Katika mradi uliozinduliwa, Kampuni ya simu za mkononi nchini ya Airtel wanashirikiana na Shirika la umoja wa mataifa la kuhudumia watoto UNICEF.

Aidha kwenye utekelezaji wake utaunganisha shule za Sekondari 3,000 na mtandao wa Airtel 4G kuwezesha upatikanaji bure wa maudhui ya kujifunza Kidijitali kutoka Maktaba mtandao ya Mamlaka ya Elimu Tanzania (TET).

Waziri Mkuu Majaliwa amesema kwamba, kujifunza kidigitali ndio njia ya haraka zaidi ya kuboresha matokeo ya kujifunza na kuandaa vijana huku akibainisha kwa sasa uwiano wa vitabu kwa mwanafunzi katika shule nyingi haukidhi viwango vilivyowekwa na Serikali.

Aidha Majaliwa ameipongeza Airtel Tanzania na UNICEF kwa kuendeleza mpango huo wa Airtel SmartWasomi unaosaidia juhudi za Serikali kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa elimu kwa vijana nchini.

Katika hotuba yake, Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania, Dinesh Balsingh alisema, kwenye utekelezaji mradi utaunganisha shule za Sekondari 3,000 na mtandao wa 4G kuwezesha upatikanaji bure wa maudhui ya kujifunza Kidijitali kutoka Maktaba mtandao ya Mamlaka ya elimu Tanzania (TET).

Balsingh alisema kwamba, mpango wa Airtel SmartWasomi umekuwa na mafanikio katika awamu ya majaribio na tayari imeunganisha shule 50 za Sekondari zilizopo Zanzibar,Dodoma na Mbeya.

Alisema kuwa, mafunzo yametolewa kwa walimu zaidi ya 2,000 na hivyo kuwafikia wanafunzi zaidi ya 55,000 wanaofundishwa na walimu hao na kwamba mradi umefanya upembuzi wa kujua hali ya upatikanaji mtandao wa Intaneti ya Airtel 4G kwa shule 4,200 na 500 huko Zanzibar.


Aidha Balsingh alisema kuwa, Airtel imeondoa malipo ya bando ili kuwawezesha wanafunzi na walimu kusoma bure bila malipo ya Intanet kwenye Maktaba ya mtandao ya taasisi ya elimu Tanzania na shule.


Kwa mujibu wa Balsingh, Airtel Tanzania ilianza utekelezaji dhamira yake ya kusaidia elimu Kidijitali 2015 kwa kuzindua mradi wa VSOMO ikishirikiana na mamlaka ya mafunzo ya ufundi stadi Veta.


Alibainisha kuwa utaratibu huo umekuwa ukifanyika kupitia aplikesheni iliyopo kwenye Simu janja inayowezesha upatikanaji w kozi ya Veta bila kuwa na haja kuhudhuria darasani.


Pia ameieleza Airtel kwamba, imekuwa na ushirikiano na DTB kwa kuzindua maabara ya Kidijitali inayowajenga vijana na Wajasiriamali uwezo wa Tehama ili kuweza kusimamia biashara zao kifanisi.


Naye Adolph Mkenda, Waziri wa elimu, Sayansi na teknolojia alisema, licha ya Airtel SmartWasomi kupunguza mgawanyiko Kidijitali itaongeza tija kwa wanafunzi kuendelea kujifunza kupitia mtandao wa kasi utakaotoa huduma bure kwa wanafunzi kupitia maudhui ya Kidijitali kutoka Maktaba mtandao ya Mamlaka ya elimu.


Vile vile Waziri wa elimu, Mkenda alisema; "Mpango huu utasaidia kuongeza viwango vya ufaulu na ubora wa elimu, bila shaka utaweza kusaidia kuimarisha vijana wetu".


Kwa upande wake Aneth Komba ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya elimu Tanzania alisema,program ya SmartWasomi inatekelezwa na wizara tatu ambazo ni ile ya elimu,ofisi ya Rais Tamisemi pamoja na wizara ya Habari.


Alisema kuwa,lengo la mradi ni kuimarisha matumizi ya Tehama katika ujifunzaji na ufundishaji na kwa kuanzia taasisi ya elimu imeanzisha maktaba mtandao iliyowekwa vitabu vyote vya kinda na ziada.


Mkurugenzi huyo alisema,Kampuni ya Airtel Tanzania imeondoa gharama zote za bando na intaneti na hivyo maktaba mtandao inapatikana bila gharama ambapo matarajio ni walimu kuweza kutumia kuwasaidia wanafunzi na kupunguza changamoto ya uhaba wa vitabu shuleni.

Post a Comment

0 Comments