Ticker

6/recent/ticker-posts

VIJANA 64 WAKAMATWA MTANDAO WA Q-NET


Na Hamida Kamchalla, TANGA.

VIJANA wapatao 64 kutoka Mikoa mbalimbali nchini wamekamatwa na jeshi la polisi Mkoa wa Tanga wakiwa wanajihusisha na uhalifu wa biashara isiyo halali ya kimtandao unajulikana kama Q-net.

Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama, ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga Balozi, Dkt. Batilda Buriani amesema vijana hao wamekuwa wakiwapigia simu wazazi na kuwataka kutoa fedha ili vijana wao waweze kupata ajira kupitia bidhaa zao wanazouza.

Dkt. Buriani amefafanua kuwa vijana hao wakiwemo wavulana 29 na wasichana 35, viongozi wao wapo jijini Dar es salaam wakati mikoani wakiwatuma wao kufanya kazi hiyo.

"Tumeona vijana ambao ndiyo nguvu kazi ya Taifa, kuanzia miaka 19 hadi 24 na wengine wamefika hadi vyuo vikuu, lakini hakuna wanachofanya, kazi ni hiyo ya utapeli" amesema.

Aidha Dkt. Buriani ametoa rai kwa wazazi kuwa makini endapo kama watapigiwa simu na watu wasiowajua wakidai kutoa nafasi za ajira hasa za kimtandao.

"Huu utaratibu wa wazazi mnapigiwa simu kuna nafasi za kazi na ninyi mnawaruhusu wanakwenda, huu ni utapeli mtupu tuweni makini hasa na mitandao" amebainisha.

Hata hivyo mkuu huyo amesema kuwa vijana wote waliokamatwa watasaidiwa kupatiwa mafunzo katika vyuo vya veta ili kuweza kupata elimu ya ujasiriamali itakayowasaidia kupata ujuzi katika maeneo yao.

"Tanga ni Mkoa salama na hakuna nafasi ya kufanya biashara ambazo hazitambuliki, lakini pia vijana hawa watarudishwa katika maeneo yao chini ya uangalizi maalumu" amesisitiza.

Post a Comment

0 Comments