Angela Msimbira TABORA
NAIBU WAZIRI Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.Zainab Katimba amemtaka mkandarasi Chongqing International construction Corparation (CICO) kuhakikisha anafanya kazi usiku na mchana ujenzi wa mradi wa Tactic ili kufikia kiwango cha utekelezaji wa mradi kwa mujibu wa mkataba.
Ametoa maelekezo hayo leo juni 9,2024 alipotembelea ujenzi wa barabara ya Swetu inayojengwa kupitia mradi wa TACTIC katika Halmashauri ya Manispaa ya Tabora,Mkoani Tabora.
Katimba amesema kwa mujibu wa ratiba mkandarasi huyo anatakiwa kuwa amefikia asilimia 40 ya utekelezaji wa mradi lakini mpaka sasa amefikia asilimia 8.6
'Tunataka kuona kasi ya ujenzi ili kufikia asilimia ya utekelezaji wa mradi iliyokubalika kwenye mikataba kwa kuwa mkifanya tofauti mnakuwa mmevunja mkataba' amesisitiza Katimba
Katimba ametoa siku 30 za matazamio kwa mkandarasi huyo kuanzia juni 8,2024 ili kukamilisha utekelezaji wa miradi kulingana na ratiba iliyowekwa kwenye mkataba
Amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan anatafuta fedha kwa ajili ya kuwahudumia wananchi,hivyo ni jukumu la mkandarasi kuhakikisha anatimiza majukumu yake kimkataba.
'Hatubembelezi wala hatuombi kwa kuwa serikali imeshatimiza jukumu lake hivyo ni wajibu wa mkandarasi kukamilisha kazi kwa wakati kama ilivyokubalika kwenye mkataba,'" amesisitiza Mhe. Katimba
Naye Mkuu wa Wilaya ya Tabora Mjini Mhe. Deusdedit Katwale amemtaka mhandisi mshauri UNITEC CIVIl Consultants Ltd kuhakikisha anasimamia taratibu kwa kuwa yeye ndiye aliyewekwa na Serikali katika usimamizi wa mradi huo na kuchukua hatua kwa mkandarasi kwa mujibu wa sheria, taratibu na miongozo ya serikali.
Ameitaka Halmashauri ya manispaa ya Tabora kuhakikisha wanachagua wakandarasi wenye uwezo wa kazi na kuacha tabia ya kuchagua wakandarasi wwnye gharama ndogo.
'Katika miradi mikubwa kama hii ni vyema tukaangalia uwezo wa mkandarasi, vifaa anavyotumia na umahiri wa kazi,tujiepushe kuchukua wakandarasi ambao gharama zao ni za chini ambao mara nyingi huchelewesha ukamilishaji wa miradi kwa wakati' amesisitiza Mhe. Katwale
Mhandisi wa Wakala wa barabara vijijini na mijini Subira Manyama amesema kuwa jumla ya shilingi bilioni 16.5 zitatumika kwa ajili ya ujenzi wa barabara zenye urefu wa km 10.7.
Amesema,mkandarasi huyo ameingia mkataba wa ujenzi wa barabara ya mkunazini -madaraka Kanon kisarika,Malitano,swetu ujenzi wa Jango la ofisi ya mhandisi ambavyo vote hivyo vimetekelezwa kwa asilimia 8.6
Aidha,Halmashauri ya Manispaa ya Tabora ni miongoni mwa halmashauri 12 zilizoingia kwenye mradi wa TACTC kwa kigezo cha idadi kubwa ya watu na ukuaji wa miji kwa mujibu w sensa ya mwaka 2012.
0 Comments