Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema ajenda ya kutumia nishati safi ya kupikia ni ya muhimu ili kuokoa maisha ya watu na mazingira.
Amesema hayo wakati wa mkutano wa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu Bi. Zuhura Yunus pamoja na viongozi wengine na Vyombo vya Habari, Ikulu jijini Dar es Salaam leo tarehe 17 Mei, 2024 kuhusu Mkutano wa Nishati Safi ya Kupikia uliofanyika jijini Paris nchini Ufaransa.
Dkt. Jafo ameeleza kuwa Mkutano wa Nishati Safi ya Kupikia umefanikiwa kwa asilimia kubwa chini ya Kinara wa Nishati Safi ya Kupikia Afrika, Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na wenyeviti wenza, wamewezesha upatikanaji wa Dola za Kimarekani bilioni 2.2.
Pia, amesema Uingereza imeahidi kutoa Dola za Kimarekani 3.4 milioni kwa Tanzania, ambapo ni mafanikio yaliyopatikana katika mkutano huo ambapo ni fursa kwa nchi katika kuchagiza matumizi ya nishati safi ya kupikia, hatua itakayowasaidia akinamama na wasichana kuzalisha na kusoma badala ya kutafuta kuni.
Waziri Jafo amesema Tanzania imejipambanua katika ajenda ya nishati safi kwa kuwa na Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ambao ni nyenzo muhimu ya kukabiliana na athari za kimazingira, kiafya, kijamii na kiuchumi.
Amesema Serikali inashirikisha sekta binafsi katika ajenda ya nishati safi kuhakikisha uwezo wa wananchi katika kumudu, upatikanaji na kujenga uelewa kwa wananchi kutumia nishati safi badala ya kuni na mkaa.
Halikadhalika, amesema maelekezo ya Serikali kwa taasisi zinazolisha zaidi ya watu 100 kuacha kutumia kuni na mkaa katika kuandaa chakula ni mojawapo ya mikakati ya kuhifadhi misitu ambayo takwimu zinaonesha zaidi ya hekta laki nne zinapotea kila mwaka kutokana na ukataji wa miti.
“Kutokana na uharibifu wa mazingira unaotokana na ukataji wa miti tuna kazi kubwa ya kufanya, kwanza lazima tuhame twende katika nishati safi ya kupikia na *kwa* uzinduzi wa mkakati wa nishati safi ya kupikia tuna afua mbalimbali zinatekelezwa kuhakikisha kwamba suala la uharibifu wa mazingira,” amesema.
Aidha, Dkt. Jafo amesema kuwa pamoja na mikakati hiyo pia Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais inaendelea kusimamia utekelezaji wa zoezi la upandaji wa miti katika kila Halmashauri ambapo imeelekezwa zipande miti milioni 1.5 kila mwaka.
Amewahimiza wananchi na taasisi kupanda miti na kuitunza kwani katika lengo la Serikali la kupanda miti milioni 266 kwa Halmashauri zote ni miti milioni 211 sawa na asilimia 76.5 ndio imestawi.
0 Comments