Ticker

6/recent/ticker-posts

WASHINDI WA SHINDANO LA WAUZAJI BORA WA VILAINISHI VYA ORYX WAZAWADIWA TIKETI ZA KWENDA DUBAI

Na Mwandishi Wetu

BAADA ya Kampuni ya Oryx Services and Specialties Ltd kukabidhi tiketi za kwenda Dubai pamoja na kugharamia kila kitu kwa washindi wawili wa Shindano la Wauzaji Bora wa Vilainishi vya Kampuni hiyo(Mawakala) wamesema kwao kupata safari hiyo kunakwenda kuongeza ari na kasi katika kuendelea kuuza na kutafuta masoko kwa ajili ya kuuza vilainishi hivyo.

Wakizungumza leo Mei 31,2024 jijini Dar es Salaam baada ya kukabidhiwa tiketi zao wamesema ushindani ulikuwa mkubwa kutoka kwa mawakala wengine zaidi ya 50 waliokuwa wakishindana lakini wao wameibuka washindi na hatimaye wamekabidhiwa tiketi za kwenda Dubai kwa siku nne.

Mmoja wa washindi hao Vaileth Cilwimba kutoka Lwimba Investment Company Ltd jijini Dar es salaam (Msambazaji) ameeleza kuwa wanaushukuru kwa kushinda shindano hilo lakini wao wamekuwa wakijivunia kuuza bidhaa bora za vilainishi vya Oryx.

"Tunashukuru kwa kushinda na kupata tiketi kwa ajili ya kwenda Dubai ambapo tumelipiwa kila kitu kwa maana ya gharama zote, kwetu hii inatufanya tuongezee bidii zaidi kwa kuuza zaidi bidhaa bora za Oryx zikiwemo za Vilainishi vya magari,bodaboda, bajaji na mitambo mbalimbali."

Akizungumza baada ya kukabidhi tiketi kwa washindi hao, Mkurugenzi Mkuu wa Oryx Energies Tanzania Kalpesh Mehta amefafanua Oryx Services and Specialties Ltd iliendesha shindano la wauzaji (mawakala) bora wa vilainishi vya Oryx Energies kati ya Maduka ya Oryx na wasambazaji wa Vilainishi vya Oryx.

Amefafanua shindano hilo lilianza Januari na kumalizika Desemba 2023 ,hivyo leo Mei 31, 2024 wametangaza washindi wa shindano Mbise Oil Shop iliyopo Arusha (Oryx Shop) pamoja na Lwimba Investment Company Ltd iliyopo Dar es salaam (Msambazaji).

"Zawadi kwa washindi wa shindano hili ni Safari ya kwenda Dubai kwa siku nne,mbali ya tiketi ambazo tunakabidhi hapa watagharamiwa kila kitu,ni safari nzuri na wakiwa huko watapata nafasi ya kutembelea maeneo mbalimbali.Kila mshindi amepata tiketi mbili kwa ajili ya safari ya Dubai."

Ameongeza pia wanatarajia kutangaza mashindano mengine kama hao hivi karibuni na kusisitiza kwamba yatakuwa ya kusisimua zaidi kuliko shindano lililopita.Hivyo ni matumaini yao wauzaji wao wote watashiriki tena vyema kama mwaka uliopita.

"Oryx Energies ni kampuni kubwa na ya muda mrefu ya kimataifa inayotoa huduma za nishati barani Afrika. Oryx Energies huagiza, kuchakata, huhifadhi na kusambaza bidhaa za mafuta ya magari, machine na mitambo (Dizeli, Petroli, Vilainishi) na gesi za kupikia (LPG) zitumikazo katika sekta mbalimbali za uchumi.

"Ni msambazaji namba moja wa bidhaa za mafuta na vilainishi katika sekta ya uchimbaji madini (migodi). Pia Oryx Energies inaongoza kusambaza vilainishi katika sekta zingine za kiuchumi kama usafirishaji wa nchi kavu (pikipiki, magari, treni) na majini, viwandani, ujenzi na kilimo.

Pia amesema katika kuhakikisha bidhaa na huduma zinapatikana kwa watumiaji kote nchini, Oryx Energies inaendelea kuboresha njia zake za usambazaji kwa kupitia Maduka ya Kipekee ya Kampuni (CODOs), Wasambazaji na vituo vya mafuta vya Oryx.

Wakati huo huo Arthur Awet ambaye ni B2C Key Account Manager Kampuni ya Oryx Services and Specialties Ltd wakati anaeleza Mashindano hayo amesema Oryx Services and Specialties LTD iliendesha shindano ya CODO na wasambazaji wao 50 ya kutafuta mtendaji bora wa mauzo katika bidhaa zao zote za vilainishi.

Mkurugenzi Mkuu wa Oryx Energies Tanzania Kalpesh Mehta akimkabidhi mfano wa zawadi ya tiketi ya Safari ya kwenda Dubai Vaileth Cilwimba kutoka Lwimba Investment Company Ltd jijini  Dar es salaam (Msambazaji) ambaye ni mshindi wa shindano la wauzaji (mawakala) bora wa vilainishi vya Oryx Energies kati ya Maduka ya Oryx na wasambazaji wa Vilainishi vya Oryx. Zozi la ugawaji wa tiketi hizo limefanyika leo Mei 31,2024 Jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mkuu wa Oryx Energies Tanzania Kalpesh Mehta akimkabidhi mfano wa zawadi ya tiketi ya Safari ya kwenda Dubai  Mwakilishi wa Kampuni ya Mbise Oil Shop iliyopo Arusha (Oryx Shop)(Msambazaji) ambaye ni mshindi wa shindano la wauzaji (mawakala) bora wa vilainishi vya Oryx Energies kati ya Maduka ya Oryx na wasambazaji wa Vilainishi vya Oryx. Zozi la ugawaji wa tiketi hizo limefanyika leo Mei 31,2024 Jijini Dar es Salaam.

Post a Comment

0 Comments