Ticker

6/recent/ticker-posts

WANASAYANSI VYUO VYA NDANI KULIPIWA NA SERIKALI, BILA MIKOPO.


Na Hamida Kamchalla, TANGA.

SERIKALI imesema wanafunzi wapatao 600 hadi 700 wanaofuzu vizuri masomo ya sayansi na kutaka kusoma vyuo vya ndani ya nchi watasomeshwa bure.

Wanafunzi hao ni wale watakaosoma masomo ya sayansi, uhandisi, tehama, elimu tiba na hisabati ambao hawatakuwa na garama za kulipia kwani kwa asilimia 100 watalipiwa na serikali.

Waziri wa Elimu na Prof. Adolf Mkenda amebainisha wakati akizindua maadhimisho ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yaliyofanyika Kitaifa jijini Tanga.

"Siyo mikopo, serikali itakulipia garama zote ikiwemo kujikimu, malazi na chakula mpaka umalize kusoma, ilimradi waendelee kufanya vizuri kwenye masomo yao kwenye vyuo wanavyosomea" alisema Prof. Mkenda.

Amebainisha kwamba kupitia ilani ya uchaguzi katika kuendeleza sayansi na tekinolojia, Rais aliagiza zitengwe fedha kwa ajili ya kuwasomesha vijana wanaofanya vizuri sana katika masomo ya sayansi.

Waziri huyo pia amesema serikali ipo katika mchakato wa kujenga shule 100 za mafunzo ya Amali katika nyanja ya ufundi nchi nzima ili kuwawezesha vijana wa Kitanzania kuweza kujiajiri au kuajiriwa kupitia ujuzi watakaopata kupitia vyuo hivyo.

Hata hivyo Prof Mkenda amezindua rasmi mwongozo wa Samia Scholarship kwenda kusomea elimu ya juu ya nyuklia nje ya nchi ikiwa ni pamoja na kuongeza madirisha ya wanataka kwenda kusoma nje ya nchi.

Waziri Prof. Mkenda pia amesema maonesho hayo ni chachu ya maendeleo kwa sekta ya elimu katika ubunifu na kusisitiza kwamba, wenye bunifu zao wajipange na kuwania fursa ,ilizipo kwenye maadhimisho hayo.

"Watu wote wenye bunifu zao wajipange na wakae tayari kwani maonesho haya yatafanyika kila mwaka, na yatafanyika walau kwa miaka miatatu katika Mkoa huu, usilalamike fursa ipo njoo uoneshe ubunifu wako".

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi amesema ili kuendana na kasi ya maendeleo Duniani inapasa kufanya mabadiliko makubwa ya sayansi na tekinolojia

"Dunia ya sasa ina mabadiliko makubwa hasa kwenye masuala ya sayansi, tekinolojia, Ujuzi na Ubunifu, hivyo basi ni wakati wa vijana wa Kitanzania kwenda sambamba na mabadiliko hayo" amesema.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Elimu, Husna Sekiboko amesema Bunge linatamani kuona bunifu zinazoibuliwa zinaboreshwa Ili zilete tija na kutatua kero mbalimbali za kijamii

"Muhimuli huu unataka kuona bunifu zinazoibuliwa hazibaki kwenye maonesho pekee bali ziendelezwe na kufikia hatua ya kubiasharishwa ili kichochea maendeleo ya kiuchumi na kutoka hamasa kwa wabunifu mbalimbali,

"Maonesho haya yameibua fursa mbalimbali kwa wananchi wa Mkoa wa Tanga na wadau wa maendeleo ambayo wamejifunza tekinolojia mbalimbali za kisiasa katika kutekeleza majukumu yao" amesema Sekiboko.

Post a Comment

0 Comments