Ticker

6/recent/ticker-posts

WAKUU WA VYUO WAHIMIZWA KUSAIDIA NACTVET KUTIMIZA MALENGO YA KITAIFA


Na Okuly Julius , Dodoma

Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET), Dkt. Adolf Rutayuga, leo tarehe 10 Mei 2024 amewarai Wakuu wa vyuo vya kati kusaidia juhudi za Baraza kutekeleza majukumu yake ya urekebu kwa maslahi ya vyuo na wanavyuo.


Dkt. Rutayuga amesema hayo wakati wa warsha ya wadau wa vyuo vya elimu ya kati, wakiwemo wakuu wa vyuo na maafisa udahili vyuoni. Amesema vyuo havina budi kuzingatia taratibu, kanuni na miongozo ya udahili, ufundishaji wa programu, upimaji na utunuku inayosimamiwa na NACTVET, ili kupunguza changamoto zinazojitokeza mara kwa mara kwenye matokeo ya upimaji.



Dkt. Rutayuga pia amewataka wakuu wa vyuo kuhimiza wahasibu wao kuwasilisha ada ya udhibiti ubora vyuoni, ili kuliwezesha Baraza kutuma watendaji wake kwenye kaguzi za vyuo.


Aidha, kuhusu maboresho kwenye ufundishaji mitaala inayozingstia umahiri (CBET), Dkt. Rutayuga amesema tayari Baraza limejenga mfumo utakaowawezesha walimu kujenga uwezo wao katika kufundisha mitaala ya umahiri, kwa kujisajili mtandaoni na kupata mafunzo hayo hadi kuhitimu.


Ameshauri walimu kujisajili na mfumo huo ili vyuo viwe na waalimu wenye uwezo kufundisha programu husika kwa uhakika zaidi.


Kwa upande wa taarifa za wanavyuo (data) walio kwenye mfumo wa vyuo, Dkt. Rutayuga amehimiza vyuo kuhakikisha mifumo yao ya TEHAMA inasomana na mfumo wa NACTVET, ili kupunguza changamoto ya wanavyuo kusoma wakiwa nje ya mfumo wa Baraza.



Wakati huo huo, Meneja Utahini na Utunuku wa NACTVET, bw. Twaha Twaha amevitaka vyuo kuhakikisha taarifa za wanavyuo zinafika kwenye mfumo wa Baraza kwa wakati ili wanavyuo waweze kukidhi sifa za kutahiniwa ili wapate utunuku stahiki mwisho wa muhula wa masomo.


Warsha hiyo imewakutanisha jumla ya washiriki 293 wakiwemo wakuu wa vyuo, maafisa udahili na maafisa mitihani vyuoni.

Post a Comment

0 Comments