Ticker

6/recent/ticker-posts

TANZANIA IMEPIGA HATUA KWENYE MAWASILIANO – MAJALIWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazopiga hatua kubwa kwenye sekta ya mawasiliano na teknolojia ya habari.

Amesema kuwa mipango na mikakati iliyowekwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha sekta ya teknolojia ya habari na mawasiliano inakua, imeonesha kuleta matokeo chanya katika maendeleo ya Taifa.

“Ninatoa pongezi kwa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, sasa tunaona Taifa letu linakwenda kufanikiwa kwenye mabadiliko ya teknolojia ya Habari na Mawasiliano, tumefanikiwa kufanya Serikali kuwasiliana kati ya Wizara na Wizara na kuiunganisha nchi nzima.”

Amesema hayo leo (Alhamisi Mei 16, 2024) alipotembelea mabanda ya maonesho ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwenye viwanja vya Bunge, jijini Dodoma.

Waziri Mkuu amesema kuwa hatua iliyofikiwa ya kufikisha mawasiliano kwa wananchi mpaka vijijini ni kubwa. “Kwa sasa tunakwenda kuwezesha kila Mtanzania kutumia teknolojia ya kisasa katika kuwezesha shughuli zake iwe ni biashara, masomo na namna nyingine yeyote ile ambayo inahitaji teknolojia na mawasiliano.”

Amesema kuwa Serikali inaendelea na mkakati wake wa kuhakikisha teknolojia ya habari na mawasiliano inafanya vizuri katika sekta ya elimu kuanzia vyuo vikuu hadi shule za msingi. “Tumeitaka Wizara mwaka huu wa fedha iongeze bajeti na kuimarisha eneo la sayansi na teknolojia hadi kufikia ngazi ya shule za msingi ili kuwezesha Taifa letu kupata maendeleo ya haraka kwenye sekta ya elimu.”

Aidha Mheshimiwa Majaliwa ameipongeza Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa maboresho makubwa yanayofanywa katika sekta ya habari, mawasiliano na teknolojia ya habari.

“Sisi tuna matumaini makubwa kwamba katika kipindi kifupi kijacho, kupitia bajeti ya mwaka huu, tutafanya shughuli nyingi ya kuwafanya Watanzania wawe karibu na mapinduzi ya teknolojia ya habari na mawasiliano,” amesema.

Post a Comment

0 Comments