Na Okuly Julius, Dodoma
Mwanachama wa Chama cha Mapinduzi CCM kutoka Wilaya ya Muheza mkoani Tanga , Ndg. Hamisi Sadick Rajabu ameishauri Serikali kuharakisha zoezi la upimaji wa Ardhi katika vijiji ili kutimiza adhima ya CCM kama ilivyoelekezwa kwenye Ilani kuhakikisha vijiji vyote viwe vimeshapimwa hadi kufikia 2025.
Ameyasema hayo mbele ya waandishi wa habari Mei 24 , 2024 katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma, mara baada ya kushuhudia uwasilishwaji wa Bajeti ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Ameishauri Serikali kuongeza Fedha ili kuhakikisha zoezi hilo linaharakishwa kwani kwa sasa linaonekana kusuasua.
"Serikali inafanya jitihada kubwa sana ya kuhakikisha inamaliza migogoro ya ardhi kwa hilo nalipongeza na kufanya hivyo ni kutekeleza ilani ya chama cha mapinduzi na ilani hiyo pia ilielekeza ifikapo 2025 ardhi katika vijiji vyote iwe imepimwa hivyo nitumie fursa hii kama mwanachama wa CCM kuishauri serikali iharakishe zoezi hilo kwa kuongeza fedha katika eneo hilo la upimaji ardhi," ameleeza Hamisi
Amesema kwa mjadala huo wa bajeti ya Wizara ya Ardhi ,Nyumba na Maendeleo ya Makazi inaonesha dhahiri malengo ya serikali ni kutaka wananchi wake wamiliki ardhi na kuishi katika mazingira salama na kuondoa kabisa migogoro ya ardhi ila kuhakikisha jamii inanufaika na matumizi ya ardhi.
0 Comments