NA EMMANUEL MBATILO
MBUNGE wa Jimbo la Kisesa Mheshimiwa Luhaga Mpina amesema Tanzania inaripotiwa kutorosha nje ya nchi zaidi ya Tsh Trilioni 3.5 kwa mwaka na Kenya inaripotiwa kutorosha zaidi ya Ksh 40 bilioni (sawa na Tsh Bilioni 744) kwa mwaka.
Amesema kwanini mianya ya upotevu wa mapato na raslimali za nchi imeshindwa kudhibitiwa barani Afrika?
Mpina ameyasema hayo wakati akichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 Mei 28, 2024 Bungeni Dodoma.
Amesema nchi nyingi za Afrika zimetumbukia kwenye mzigo mkubwa wa madeni (Highly Indebted Poor Countries-HIPC) na mikopo hiyo inatolewa kwa masharti magumu na ya kinyonyaji.
“Nchi nyingine kuchukua mikopo inayolindwa na dhamana ya maliasili za nchi kama madini, gesi, mafuta, bandari nk, kuingiliwa katika utungaji na Usimamizi wa sera, sheria, kanuni, miongozo, program na mikakati na hivyo kunyang’anywa uhuru wa kujiamulia mambo wakati mwingine kutekeleza miradi ambayo haipo kwenye vipaumbele vya nchi ili kukidhi matakwa ya wahisani, mikopo kukosa uwazi, ulinganifu na yenye riba kubwa na masharti mengi ya kinyonyaji na kusababisha mfumko mkubwa wa bei za bidhaa”. Ameeleza Mhe. Mpina
Aidha amesema kuwa Mikopo ya aina hiyo imezifanya nchi nyingi za Afrika kufilisika na kurudi nyuma kiuchumi na kuendelea kuishi kwa kutegemea misaada na mikopo na kupelekea kuongezeka kwa migogoro ya kifedha hasa inapotokea ugumu wa kurejesha mikopo hiyo.
“Kwanini nchi za Afrika zimeshindwa kujenga uchumi imara na kuendelea kutegemea misaada na mikopo. Bw. Donald Kaberuka, Gwiji wa uchumi huko nchini Rwanda aliwahi kusema waafrika tunatakiwa kugundua namna ya kutumia raslimali zilizopo katika bara ya Afrika ili kuibadilisha Afrika”. Amehoji Mhe. Mpina.
0 Comments