Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk amekutana na kuzungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia Balozi Birtukan Ayano ofisini kwake Mtumba jijini Dodoma.
Katika mazungumzo yao viongozi hao wamekubaliana kuendelea kuimarisha uhusiano uliopo kati ya Tanzania na Ethiopia kwa manufaa ya pande zote mbili.
Akizungumza na mgeni wake Mhe. Balozi Mbarouk amesema Tanzania inajivunia kuwa na uhusiano na ushirikiano imara na Ethiopia hali ambayo inazifanya nchi hizo kuendelea kushirikiana katika sekta za usafiri wa anga, nishati, Kilimo, Mifugo, Utalii, Ulinzi na Uhamiaji
Balozi Mbarouk amesema Tanzania itatumia uhusiano wake na Ethiopia kukuza biashara na uwekezaji kwa manufaa ya pande zote mbili.
Balozi Mbarouk pia ameipongeza Ethiopia kwa kuwa nchi ya kwanza kuweka jiwe la msingi kwa ajili ya Ujenzi wa Ofisi zake za Ubalozini na makazi ya Balozi katika eneo ambalo Ethiopia ilipewa na Serikali ya Tanzania.
Akizungumza katika kikao hicho Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia Balozi Ayano amesema Ethiopia inaiona Tanzania Kama mdau muhimu wa kushirikiana naye kwa lengo la kukuza biashara na uwekezaji na kuendeleza uhusiano uliopo.
Amesema amekuja Tanzania pamoja na masuala mengine kwa kazi ya kuweka jiwe la msingi kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Ofisi za Ubalozi na makazi ya Balozi wao katika makao makuu ya Tanzania jijini Dodoma.
“Ethiopia ni makao makuu ya Umoja wa Afrika , sisi ni viongozi na tunataka kuwa mfano kwa nchi za Afrika na nyingine kwa kuwa wa kwanza kuwa na jengo letu hapa Mtumba,” alisema Balozi Ayano.
Ameongeza kuwa Ethiopia inaamini kuwa kitendo hicho cha kuweka jiwe la msingi na kuanza Ujenzi wa majengo hayo kitaendelea kuimarisha uhusiano wake na Tanzania.
Ethiopia inakuwa nchi ya kwanza kuweka jiwe la msingi kwa ajili ya Ujenzi wa Ofisi za Ubalozi na makazi ya Balozi tangu Serikali ya Tanzania ilipohamia jijini Dodoma Makao Makuu ya Serikali mwaka 2017.
China, Ujerumani, Ufaransa, Uingereza , Marekani na Umoja wa Mataifa na Mashirika yake yana Ofisi ndogo jijini Dodoma zilizofunguliwa baada ya Serikali kuhamia jijini Dodoma.
0 Comments