Ticker

6/recent/ticker-posts

UDSM KUADHIMISHA MAADHIMISHO YA TISA YA WIKI YA UTAFITI NA UBUNIFU 2024

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

CHUO Kikuu Cha Dar es Salaam kinatarajia kuadhimisha maadhimisho ya Tisa ya Wiki ya Utafiti na Ubunifu kwa mwaka 2024 ambayo yanatarajiwa kuanza kwa ngazi ya vitendo (ndaki, shule kuu na taasisi) kuanzia tarehe 17 hadi 19 Aprili 2024 na kumalizikia katika ngazi ya Chuo kuanzia tarehe 5 hadi 7 Juni 2024.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 9,2024 Jijini Dar es Salaam, Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo-Utafiti Prof. Nelson Boniface amesema maadhimisho hayo yatatoa fursa kwa wadau na washirika wanaopenda kuingia ubia na Chuo katika kutumia matokeo ya tafiti na ubunifu mbalimbali kibiashara au kushiriki katika huduma za ushauri.

"Hii itaimarisha ushirikiano na kuzidi kugeuza utafiti na ubunifu kuwa manufaa yanayoonekana katika jamii". Amesema

Aidha Prof. Boniface amesema kuwa maadhimisho ya mwaka huu 2024 yanatambua umuhimu wa ushirikiano kupitia ubia baina ya UDSM na Tasnia mbalimbali (Industry).

Amesema maadhimisho ya tisa na Utafiti na Ubunifu yatatoa nafasi muhimu kwa wadau wa ndani na nje kuona mchango wa ushirikiano huu na kutambua thamani kubwa ya juhudi za utafiti na ubunifu za UDSM.

Pamoja na hayo amesema Maadhimisho hayo yatakuwa ni fursa adhimu ya kusambaza matokeo na kuonesha ubunifu, kuongeza uelewa miongoni mwa wadau na umma kwa ujumla kuhusu nafasi ya Chuo katika kuchagiza maendeleo ya nchi na jamii kwa ujumla.

Ameeleza kuwa maadhimisho hayo pia yatatumika kutambua michango ya wanataaluma na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika utafiti, ubunifu na ubadilishanaji wa maarifa.

"Siku ya kilele cha maadhimisho haya ambayo itakuwa tarehe 7 Juni 2024, kutatolewa tuzo kwa watafiti na wabunifu bora katika makundi mbalimbali". Amesema Prof. Boniface.

Kaulimbiu ya Maadhimisho haya ya tisa ni Kukuza Utafiti na Ubunifu kupitia Ubia baina ya Chuo na Tasnia Mbalimbali.
Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo-Utafiti Prof. Nelson Boniface (katikati)  akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 9,2024 katika ukumbi wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam.

Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo-Utafiti Prof. Nelson Boniface akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 9,2024 katika ukumbi wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam.

Post a Comment

0 Comments