Ticker

6/recent/ticker-posts

MAFUNZO YA USALAMA BARABARANI KUPUNGUZA AJALI ZA MADEREVA BODABODA MKOANI TANGA

Na Mwandishi Wetu,Korogwe

JESHI la Polisi Kikosi cha Usalama barabarani Mkoa wa Tanga limesema madereva bodaboda watano mpaka 10 wanapoteza maisha kwa siku katika Mkoa huo na wengine wanapata ulemavu kutokana na ajali za barabarani.

Kwa mujibu wa Jeshi hilo ajali hizo zinasababishwa na madereva hao kutozingatia Sheria za usalama barabarani,hivyo uwepo wa mradi wa mafunzo ya usalama barabarani kwa madereva bodaboda unaotekelezwa na Shirika la Amend kwa kushirikiana na Ubalozi wa Uswisi nchini umesaidia kupunguza ajali hizo.

Hayo yamesemwa na Kaimu Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Tanga (RTO) Hamis Mbilikila alipokuwa akitoa elimu ya mafunzo ya usalama barabarani kwa madereva bodaboda wa eneo la Hale wilayani Korogwe mkoani Tanga.

Amesema hali hiyo inachangia kwa asilimia kubwa kusababisha kupoteza nguvu kazi kubwa ya vijana kutokana na asilimia kubwa kujiajiri kupitia sekta hiyo bila kuwa na elimu ya sheria za usalama barabarani wakati wakitekeleza majukumu yao ya kila siku.

"Kwa sehemu kubwa ajali hizi zinasababishwa na watumiaji wa vyombo vya moto asilimia kubwa kutozingatia sheria za usalama barabarani.Hivyo uwepo wa mafunzo hayo ambayo yanatolewa na Amend kwa mkoa wetu yatasaidia kupunguza ajali zinazotokana na madereva hao wa pikipiki maarufu kama bodaboda."

Hivyo amesema mafunzo hayo wanaamini yatakuwa na tija ka madereva hao ambao huku akiwataka pia kuacha kujichukulia sheria mkononi pindi ajali zinazopotekea kweye maeneo yao badala yake watoe taarifa kwenye mamlaka husika.

Amewakumbusha bodaboda ajali zinapotokea wasichukue sheria mkonono,ni vema wakatoa taarifa mkoa wa Tanga ambao ni Mkoa wa kimkakati kwani kuna mambo mengi yanafanyika.

"Kuna bomba la mafuta ,kuna wageni wengi katika bandari yetu ambayo pia imefunguka ,kuna njia inaunganisha nchi jirani na Kenya na hapa hale ni barabara kuu kuna watu wengi wanapita hivyo ni lazima tufuate sheria za usalama barabara,”amesema Mbilikila.

Kwa upande wake Ofisa Miradi kutoka Shirika la Amend Tanzania akizungumza wakati wa mafunzo hayo Scolastica Mbilinyi amesema lengo lao ni kupeleka mafunzo kwenye maeneo mbalimbali ili kuwafikia watu wengi kupitia kampeni ya usalama barabarani .

Ambapo amesema kwa sasa wanayafikia maeneo ya pembezoni ambao ni mpango kazi wa dunia kupunguza ajali angalau kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2030.

“Tulianza Wilaya Tanga na baadae Mkanyageni wilayani Muheza na leo tupo Hale wilaya ya Korogwe.Tumepanga kupeleka elimu hii kwenye maeneo mengi kwa sababu wengi hawana elimu ya usalama barabarani na itasaidia kuokoa maisha ya watu wengi zaidi baada ya kupata elimu hii."

Amewataka bodaboda kufuata sheria za usalama barabarani ikiwemo kutembea mwendo unaotakiwa kulingana na alama za barabarani zinavyoelekeza sambamba na pikipiki zao kuwa zimekamilika ili kupunguza ajali.

Pia amesema wanatoa elimu ya usalama barabarani kwa shule za sekondari,msingi na kwenye jamii wakiwemo madereva wa pikipiki maarufu bodabda na wamekuwa wakishirikiana na Jeshi la Polisi kufanikisha mafunzo hayo.

Awali Mratibu wa Shirika la Amend Tanzania Ramadhani Nyanza amewashakuru bodaboda kwa mwitiko wao mzuri kwani wamejitokeza kwa wingi huku akieleza mikakati yao baada ya kutoka Hale mafunzo hayo yatatolewa Korogwe,Mombo, Segera, Handeni na Kilindi.

Naye mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo Isa Juma ambaye ni bodaboda kituo cha Hale amesema wanashukuru wamepata elimu hiyo na kuna mambo mengi wamejifunza ambayo watayatumia ili kuondokana na ajali za barabarani.

Post a Comment

0 Comments