Ticker

6/recent/ticker-posts

KAMATI YA BUNGE YABARIKI KUANZISHWA KWA BENKI YA TAIFA YA USHIRIKA

  

Moshi. Tarehe 21 Aprili 2024: Ikiwa imebaki chini ya miezi miwili kabla Rais Samia Suluhu Hassan hajaizindua Benki ya Taifa ya Ushirika Tanzania (CBT), Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo imebariki mpango huo na kutaka ukamilishwe kwa wakati huku Benki ya CRDB ikiomba iongezewe nafasi ya kuwekeza zaidi katika benki hiyo mpya inayotarajiwa kuwahudumia zaidi wakulima hasa waliopo kwenye vyama vya ushirika.

Baraka za kuanzishwa kwa benki hiyo zimetolewa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, Mheshimiwa Mariamu Mzuzuri aliyewaongoza wajumbe wa kamati hiyo kupata taarifa za maendeleo ya mchakato ulioanza tangu mwaka 2012 wa kuanzisha Benki ya Taifa ya Ushirika.

Akiwakaribisha wajumbe wa kamati yake kuchangia mjadala wa kuanzishwa kwa benki hiyo mpya baada ya kusikiliza wasilisho la Meneja Mkuu wa Benki ya KCBL, Godfrey Ng’urah, Mheshimiwa Mzuzuri amepongeza maandalizi yaliyofanywa mpaka sasa na akasisistiza kuwa umakini zaidi unahitajika kuhakikisha malengo yanatimia kama yalivyopangwa.
“Kwa jinsi wasilisho hili lilivyojaa hoja za maana kwetu, naamini historia itatukumbuka kwa kuwa sehemu muhimu ya kuanzishwa kwa Benki hii ya taifa ya Ushirika. Tumeelezwa hapa jinsi gani benki za aina hii zilivyo imara katika mataifa mengine ambako wakulima wao wana uwezo mkubwa wa kiuchumi tofauti na wakulima wetu ambao wengi wanafanya kilimo cha kujikimu,” amesema Mheshimiwa Mzuzuri.


Kuhusu ombi la Benki ya CRDB kuongezewa uwekezaji ndani ya benki mpya inayosubiriwa, Mheshimiwa Mzuzuri amesema “kwa jinsi mlivyojitoa kuiwezesha Benki ya KCBL, ombi lenu linajadilika. Tutaona namna ya kufanikisha hilo kwa sababu ni jambo linalozunguzika.”


Alipopewa nafasi ya kuzungumza, Mwenyekiti wa Benki ya CRDB, Dkt Ally Laay alisema kila kitu kinaenda vyema kuiruhusu taasisi hiyo mpya ya fedha ianze kuwahudumia Watanzania lakini akaiomba kamati hiyo ya Bunge kuangalia namna wanavyoweza kuiongezea nafasi y akumiliki hisa nyingi zaidi za benki hiyo mpya.
“Idadi ya Watanzania wanaotumia huduma za benki ni ndogo sana nchini. Ripoti ya Finscope 2023 inaonyesha ni asilimia 22 tu. Lakini sote tunafahamu hapa kwamba uchumi wa taifa letu kwa kiasi kikubwa unategema kilimo lakini wakulima wengi ndio hawana akaunti kwa sababu wanaishi vijijini. Benki hii ya ushirika itasaidia kwenda kuwawezesha na wakishaimarika watakuja kwenye benki za biashara kuendeleza miradi yao,” amesema Dkt Laay.


Benki ya CRDB ilishatoa shilingi bilioni 7 ili kuinusuru Benki ya KCBL isife baada ya mtaji wake kuyumba na baada ya uwekezaji huo wa kimkakati, tayari zaidi ya shilingi bilioni 16.8 zimekusanywa ili kuanzisha benki mpya ya TCB. Dkt Laay alitumia fursa hiyo akifafanua kwamba huko nyuma KCBL na Tacoba zilikuwa hazifanyi vizuri hivyo serikali ikaiomba Benki ya CRDB iongeze mtaji kuziwezesha benki hizi. Ili kufanikisha hilo, Benki ya CRDB ilikubali kufanya hivyo na ikatoa fedha hizo kwa Benki ya KCBL pamoja na wafanyakazi watano na wajumbe wawili wa bodi.


“Fedha hizi zilitolewa si kama mkopo bali sehemu ya umiliki kwani hisa za benki hii mpya zitakapoanza kuuzwa basi zitaingizwa kwenye ununuzi wa hisa hizo na kuongeza kiasi kingine ili kufikisha asilimia 20 ya hisa zote za benki hiyo. Naomba muiunge mkono Benki ya CRDB ambayo sasa inatoa huduma Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo huku ikiwa na mpango wa kujitanu katika mataifa mengine yanayotuzunguka, iweze kununua hata zaidi ya asilimia 20 ndani ya Benki ya Taifa ya Ushirika,” amesema Dkt Laay.
Akiwasilisha mpango wa kuanzishwa kwa benki hiyo, Meneja Mkuu wa Benki ya KCBL, Godfrey Ng’urah amesema inalenga kuongeza njia mbadala za mapato kwa vyama vya ushirika, kutoa huduma zenye gharama shindani kwa kuwafikia watu wengi zaidi, na kutoa bidhaa za fedha zinazokidhi mahitaji wanachama wa ushirika.

Kuhusu manufaa yake, amesema Benki hiyo ya Taifa ya Ushirika itagusa mnyororo mzima wa thamani kuanzia masoko ya bidhaa za wakulima kuanzia wanachama wa vyama vya msingi vya ushirika, wafanyabiashara wadogo, wafugaji, wavuvi na vikundi vya Vicoba pamoja na kufanikisha miradi ya kibiashara, uzalishaji, usafirishaji na ujenzi wa maghala na ununuzi wa pembejeo za kisasa.


“Yapo malengo ya muda mrefu yaani kuanzia mwaka 2024 mpaka mwaka 2030 ya kuongeza mtaji wa Benki ya Taifa ya Ushirika ufike shilingi bilioni 100. Pamoja na Benki ya CRDB itakayomilki asilimia 20, uongozi wa KCBL unafanya mazungumzo na taasisi za nje kama Rabo Bank, IFC na AFDB na Coop Bank of Kenya kuwekeza CBT,” amesema Ng’urah.


Benki hiyo pia, amesema inakusudia kukusanya mtaji huo kwa kuuza hisa katika Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE) zitakazofanikisha kufunguliwa kwa matawi yasiyopungua 10 kutoka matatu itakayoanza nayo pamoja na kuwa na mawakala zaidiya 10,000.
Ingawa mpango wa kuanzisha Benki ya Taifa ya Ushirika ulipendekezwa mwaka 2012, mchakato wake ulichelewa kwa muda mpaka mwaka 2018 bodi ya wakurugenzi wa Benki ya KCBL iliporidhia kufanya mageuzi ya uendeshaji na ukusanyaji mtaji na mwaka 2020 bodi hiyo ikaidhinisha uwekezaji wa kimkakati wa Benki ya CRDB kutekeleza ombi la serikali.


Julai 2021, Benki ya KCBL iliidhinisha mfumo na muundo wa mageuzi kuwa Benki ya Taifa ya Ushirika na Desemba mwaka huo, Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania (TFC) iliunga mkono kuanzishwa kwa Benki ya Taifa ya Ushirika kupitia KCBL. Mwaka 2022 KCBL ilianza kupokea wanachama na fedha zilizokusanywa TFC kwa ajili ya kuanzisha benki hiyo.

Akieleza matumaini yaliyopo, Mrajisi wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Kamisheni ya Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Dkt Benson Ndiege amesema licha ya mchakato huo kuchelewa kutekelezwa tangu pendekezo lilipotolewa mwaka 2012, amesema kasi ya utekelezaji wake kwa sasa inaenda vizuri.


“Tayari Tandahimba Community Bank imebadilishwa na kuwa Tandahimba Cooperetive Bank (TCBL). Uzuri wa benki ya ushirika ni kwamba mteja ndiye mmiliki hivyo inakuwa rahisi kwao kuilinda kwa manufaa ya kizazi cha sasa na baadaye,” amesema Dkt Ndiege.

Post a Comment

0 Comments