Na Hamida Kamchalla, KOROGWE.
WATUHUMIWA 6 kati ya 13 waliotiwa mbaroni na jeshi la polisi Mkoa wa Tanga kwa madai ya kuchoma moto basi la kampuni ya Saibaba wamepandishwa kizimbani juzi machi 12, katika mahakama ya Wilaya ya Korogwe, mkoani Tanga, kujibu shitaka linalowakabili.
Katika kesi hiyo iliyoendeshwa na mwendesha mashtaka wa serikali, Sara Wangwe amemueleza hakimu msaidizi mwandamizi wa mahakama hiyo, Flora Bulijuwe kuwa watuhumiwa hao wanakabiliwa na shitaka moja.
"Shitaka lao ni moja la uharibifu wa mali kwa kuchoma moto basi la kampuni ya Saibaba lenye namba T 668 BCD, ambapo mnamo februari 27 mwaka huu, watuhumiwa walidaiwa kutenda kosa hilo kata ya Msambiazi, wilayani Korogwe' amesema.
Aidha Wangwe amewataja watuhumiwa hao kuwa ni pamoja na Bashiru Abdallah (24), Ramadhani Haruna (25), Benjamin Shehoza (24) na Abdallah Kopo (25) wakazi wa Mtonga, wengine ni Bakari Omari (24) mkazi wa Mgombezi na Bakari Anania (24) mkazi wa Kwamkole.
Kufuatia kukamilika kwa uchunguzi wa shitaka hilo, hakimu Bulijuwe amesema dhamana kwa watuhumiwa hao iko wazi ambapo kila mmoja anatakiwa kutoa pesa taslimu kiasi cha sh milioni 22.5 au hati ya mali isiyohamishika yenye thamani sawa na pesa hiyo.
"Watuhumiwa wote 6 wameshindwa kukidhi vigezo vya masharti ya dhamana na wamerudishwa mahabusu ya Wilaya hadi pale watakapokidgi vigezo hivyo" amesema Bulijuwe.
Hata hivyo, watuhumiwa hao wote wamekana kuhusika na tukio hilo ambapo hakimu Bulijuwe ameahirisha kesi hiyo hadi machi 18, 2024 itakapotajwa tena
Kabla ya kupandishwa kizimbani kwa watuhumiwa hao, awali Kamanda wa polisi Mkoa wa Tanga Almachius Mchunguzi amebainisha kuwa gari namba T. 668 BCD, Scania, mali ya kampuni ya Saibaba likiendeshwa na Seasa Chuwa (48), likitokea Dar es salaam kuelekea Arusha liligongana na pikipiki namba MC 819- EAF, aina ya Haojue iliyokuwa ikiendeshwa na Awadhi Juma (20) mkazi wa Mtonga, Korogwe.
"Ajali hiyo imeababisha majeruhi kwa dereva wa pikipiki na uharibifu wa gari, baada ya ajali kundi la watu waliokuwa wakiendesha pikipiki walifika eneo la tukio kwa lengo la kufanya uhalifu, ikiwemo kuiba mizigo ya abiria na mali zao" amebainisha.
Kamanda Mchunguzi amesema, baada ya wahalifu hao kugundua kuwa polisi wanakaribia kufika kwa ajili ya uokozi waliamua kulichoma gari hilo ambalo liliteketea kwa moto.
0 Comments