Serikali imesema ipo tayari kushirikiana na wadau wowote wenye lengo la kusaidia katika utekelezaji wa mageuzi ya Sekta ya elimu hasa katika suala la utoaji wa mafunzo ya Amali.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo Machi 8, 2024 Jijini Dar es Salaam wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na wajumbe wa Kampuni ya Kimataifa ya Miradi ya Uhandisi ya AVIC kutoka China
Prof. Nombo amesema kuwa mageuzi ya sekta ya elimu yanaangalia zaidi katika kutoa ujuzi ili kuwawezesha wahitimu wa ngazi yeyote ya elimu waweze kujiajiri, kuajiriwa, na kufungua viwanda ambavyo vitawezesha kuzalisha ajira nchini
"Napenda kuona wanafunzi tunaowapatia ujuzi wanakuwa na ubora wa kimataifa ambapo wataweza kufanya kazi mahali popote pale Duniani na ndio maana hata VETA tunataka kuona inakuwa na programu zinazotambilika kimataifa" amesisitiza Katibu Mkuu huyo
Katibu Mkuu huyo amesema kuwa katika kuhakikisha hayo yanatokea Serikali inaendelea kuwekeza na kuimarisha elimu ya amali katika shule za sekondari zinazotoa mafunzo ya amali.
Ameongeza kuwa utekelezaji wa mafunzo ya amali yanahitaji uwekezaji mkubwa katika kuhakikisha vifaa vya kisasa vya kufundishia na kujifunzia vinapatikana , hivyo wadau wanapojitokeza serikali ipo tayari kushirikiana nao kwa kufuata Sheria, taratibu na miongozo ya nchi.
Maneja wa AVIC Robin Zhu amemwambia Katibu Mkuu huyo kuwa kampuni yake kwa kushirikiana na Benki ya Exim ipo tayari katika kusaidia utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 Toleo la 2024 hasa katika upande wa kuimarisha utoaji wa elimu ya amali.
0 Comments