TANZANIA imeungana na nchi nyingine duniani kukumbuka siku ya magonjwa adimu kwa kutoa wito wa kufanyika tafiti ili kubaini vyanzo na tiba sahihi za magonjwa hayo.
Siku ya magonjwa adimu Duniani inasherehekewa kila ifikapo tarehe 29 februari ya kila mwaka na kuwa jukwaa la kuongeza uelewa kwa jamii kuhusu magonjwa hayo.
Mwanzilishi Mwenza wa Mfuko wa Kupambana na Magonjwa adimu wa Ali Kimara Rare Disease Foundation, Sharifa Mbarak alisema hayo kwenye maadhimisho ya siku hiyo yaliyofanyika siku ya Alhamisi wiki hii Jijini Dar es Salaam.
Mwanzilishi huyo alisema kwamba kupitia tafiti wataweza kubaini vyanzo vya magonjwa hayo na tiba zake.
“ni matumaini yetu kwamba tafiti za kina zinatusaidia kutambua na kubaini tiba sahihi hivyo kupunguza gharama za matibabu,”alisema Mbarak.
Mwanzilishi huyo alitoa mwito kwa serikali na wadau wa maendeleo kusaidia elimu ya nyumbani kwa watoto wenye magonjwa adimu na upatikanaji wa dawa kwa gharama nafuu.
“watoto wenye changamoto za magonjwa haya wanashindwa kuhudhuria masomo ya darasani kama wengine, hivyo kuhitaji kuwa darasa maalum kwa ajili ya kujifunza wakiwa nyumbani ni muhimu sana,”aliongeza mwanzilishi huyo.
Pia ameviomba vyuo vikuu vya tiba kuingiza magonjwa adimu kwenye mitaala yao ili kuwasaidia madaktari vijana kuweza kuyabaini katika hatua za awali.
Daktari Bingwa wa magonjwa ya watoto, Professa Karim Manji, alisema kuwa uelewa kwa jamii ni muhimu kuepusha unyanyapaa kwa wagonjwa.
Alisema kuwa watoto wengine wanaozaliwa na tatizo hili hawapati tiba sahihi na hivyo kufariki wengine wakihofia unyanyapaa na kukosa uelewa.
Kaimu Mkuu wa Chuo Cha Afya na Tiba Shirikishi Muhimbili Professa Bruno Sunguya, alisema kuwa tayari mipango iko mbioni kufanya tafiti kwa ushirikiano na vyuo vingine ili kubaini chanzo halisi na tiba sahihi.
Alisema kuwa majibu ya tafiti yatatupa majibu kwa matatizo yaliyopo na kutoa ushauri wa kisera na miongozo ya kufuatwa.
“Tunaahidi kuhakikisha tafiti zetu zinaleta matokeo ya majibu kwa magonjwa adimu ili kubaini na kupata tiba sahihi magonjwa haya,”alisema Kaimu Mkuu wa chuo.
0 Comments