Na Patrick Mabula , Kahama.
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limetoa msaada wa vifaa vya shule kwa watoto zaidi 100 wanaoishi katika mazingira magumu wanaosoma shule za msingi nne na sekondari nne zilizopo kwenye Halmashauri ya Manispaa ya Kahama.
Vifaa hivyo vilivyokabidhiwa Machi 4,2024 na Shirika la TANESCO kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ni pamoja na vifaa vya kujifunzia , madaftari na kalamu , penseli ambavyo vitawasaidia kusoma na kujifunza kwa watoto wenye uhitaji kwenye shule hizo.
Akikabidhi vifaa hivyo , Afisa Mwandamizi ,Afya na Usalama Kazini kutoka TANESCO, Nelson Mnyanyi kwenye kongamano lililofanywa na kampuni ya Jambo Group lenye kauli mbiu ya SHULE FRESH , Wakusoma Fikia Ndoto Zako lililofanyika uwanja wa Magufuli , Manispaa ya Kahama, alisema kupitia mapato linayopata Shirika la Umeme TANESCO limeamua kurudisha fadhila kwa jamii kwa kusaidia sekta ya elimu kwa kwa watoto walio kwenye mazingira magumu kwenye familia zao waweze kusoma vizuri.
Alisema Shirika la Umeme limeamua kuunga mkono jitihada za serikali kwenye sekta ya elimu na kuguswa kutoa vifaa hivyo katika kutambua umuhimu wa elimu kwa watoto waweze kusoma vizuri ili kutimiza ndoto zao.
Mgeni rasmi kwenye kongamano hilo diwani wa kata ya Majengo mjini , Benard Mahongo kwenye hotuba yake aliishukuru TANESCO na Kampuni ya Jambo Group kwa kutambua umuhimu wa elimu kwa watoto wanaosoma toka kwenye familia zenye mazingira.
Mjumbe wa Halmashauri kuu ya Jumuiya ya Wazazi ya CCM ya wilaya ya Kahama na Katibu wa elimu na Malezi na Mazingira , Shaban Mikongoti aliwataka watoto kusoma kwa bidii , nidhamu kwa kuzingatia maadili mema ambapo aliwashukuru wadau wote wa maendeleo wanaojitoa kuunga mkono jitihada za serikali kwenye sekta ya elimu.
Afisa uhusiano wa shirika la TANESCO wa mkoa wa Shinyanga , Emma Nyaki alisema mbali ya kutoa vifaa kwa watoto wa shule hizo aliwataka wasome kwa bidii kwa sababu elimu inatengeneza maisha yao ya baadae na wazingatie waliyofundishwa kuhusu usalama wa maisha katika matumizi ya umeme miongoni mwa jamii.
Naye Meneja mkuu wa Jambo Media , Nickson George wa Kampuni ya Jambo Group alisema wameendesha kongamano hilo lenye kauli mbiu ya SHULE FRESH “Wakusoma Fikia Ndoto Zako” ambapo alitoa wito kwa wadau na jamii kusaidia sekta ya elimu kwa sababu inagusa maisha ya watoto ya baadaye.
Mgeni rasmi kwenye kongamano hilo Diwani wa kata ya Majengo , Benard Mahongo akifungua kongamano hilo.
Afisa Mwandamizi wa Shirika la Tanesco , Afya na Usalama Kazini, Nelson Mnyanyi akiongea katika kongamano hilo kabla ya kukabidhi msaada .
Mjumbe wa Halmashauri kuu ya Jumuiya ya Wazazi ya CCM ya wilaya ya Kahama na Katibu wa elimu na Malezi na Mazingira , Shaban Mikongoti akizungumza kwenye kongamano hilo
Wanafunzi wa shule za msingi nne Shunu , Malunga , Bukondamoyo , Nyahanga A na za sekondari nne ambazo ni Nyashimbi , Mama Samia , Busoka na Malunga wakiwa kwenye kongamano la Jambo Media ya kampuni ya Jambo Group lenye kauli mbiu ya SHULE FRESH , Wakusoma Fikia Ndoto Zako ambako Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO ) lilikabidhi msaada wa vifaa vya shule kwa watoto zaidi 200 wanaotoka familia zenye mazingira magumu.
0 Comments