Angela Msimbira KAGERA
Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa(LAAC) imetoa siku moja kwa halmashauri zote za Mkoa wa Kagera kuainisha madai yote ya vifaa na vifaa tiba wanayoidai Bohari Kuu ya Dawa (MSD).
Agizo hilo limetolewa leo machi 17,2024 na Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Stanslaus Mabula baada ya kufika kwenye Hospitali ya Halmashauri ya Misenyi na kukuta MSD inadaiwa vifaa na vifaa tiba vyenye thamani ya Shilingi milioni 400.
“Niangize halmashauri zote za Mkoa wa Kagera kuainisha mnachoidai MSD hadi ifikapo kesho wakati wa kufanya majumuisho ili kamati ijiridhishe na kuelekeza yashughulikiwe kwa wakati.”
Kwa upande wake Meneja wa MSD Kanda ya Kagera Kalendero Masatu amesema, MSD imefanya maboresho makubwa ya kusambaza bidhaa za afya ambazo halmashauri za mkoa wa Kagera zinaidai MSD kuanzia mwaka 2021/23.
Aidha, aliyeongoza kikao cha Kamati, Mhe. Daimu Mpakate ambaye ni Mbunge wa Tunduru Kusini ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi kufanya tathmini ya mazingira kabla ya utekelezaji wa miradi kutokana na unyevunyevu unaolikabili eneo hilo.
“Hakikisheni mnatengeneza muundo mahususi kwa ajili ya ujenzi wa majengo kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi kutokana na unyevunyevu wa ardhi uliopo.”
Pia amewataka kuhakikisha wanatumia mapato ya ndani ili kukamilisha ujenzi wa shule ya Sekondari Kitoga na Hospitali ya Wilaya ya Missenyi ili majengo yatumike ipasavyo kutoa huduma kwa jamii kama ilivyokusudiwa.
Mpakate pia ameishauri halmashauri hiyo kuhakikisha wanasimamia miradi ya maendeleo kikamilifu ili kiwango cha fedha kinachotumika kiendane na ubora wa majengo yanayojengwa.
Pamoja na ushauri huo, Kamati iliupongeza uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi kwa usimamizi mzuri wa ujenzi wa miundombinu ya hospitali hiyo.
Naye, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI anayeshughulikia afya Dkt.Charles Mahera amesema TAMISEMI itaendelea kuzisimamia Mamlaka za Serikali za Mitaa nchi nzima ili ziweze kukamilisha miradi kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa ili thamani ya fedha iendane na miradi inayotekelezwa.
0 Comments