Ticker

6/recent/ticker-posts

KOICA KUONGEZA NGUVU UTEKELEZAJI MIRADI YA MAENDELEO

Na. Saidina Msangi na Peter Haule, WF, Dodoma

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Dkt. Natu El- Maamry Mwamba, amesema Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Korea (KOICA), kupitia mpango uliotiwa saini mwaka 2014 limetoa ruzuku ya jumla ya Dola za Kimarekani milioni 139.5 sawa na Sh. bilioni 356.3 kwa Tanzania kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.

Dkt. Mwamba alibainisha hayo jijini Dodoma alipokutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Korea anayeshughulikia mambo ya kimkakati (KOICA) Don Ho Kim, aliye katika ziara ya kikazi Tanzania.

Alisema kuwa kupitia fedha hizo miradi kadhaa imekamilika na mingine inaendelea ambayo ni pamoja na Mfuko wa sekta ya Afya na Mpango Jumuishi wa Vijana Walio nje ya Shule (IPOSA).

‘‘Miradi kadhaa iko katika hatua mbalimbali za maandalizi, ikiwa ni pamoja na kuanzisha mifumo ya usambazaji maji kwa maeneo ya mijini na vijijini mjini Dodoma na kuboresha usawa wa kijinsia katika Elimu (STEM) kwa Shule za Sekondari nchini ambapo miradi hii kwa sasa inapitia michakato ya kuidhinishwa ndani ya Wizara husika’’ alisema Dkt. Mwamba.

Alisema tangu 1991, KOICA imesaidia Serikali hasa katika nyanja za afya, elimu, maji na usafiri ili kubadilisha hali ya kijamii na kiuchumi nchini.

Dkt. Mwamba alisema kuwa kupitia mipango mbalimbali ya ufadhili, usaidizi wa kiufundi na programu za kujenga uwezo, KOICA imechochea mabadiliko chanya na yaliyosaidia ukuaji na ustawi jumuishi, kupambana na umaskini na kukuza uchumi.

Aidha alieleza kuwa Agosti 2023, Wizara ya Fedha iliwasilisha ombi la miradi minne ya maendeleo kwa msaada wa KOICA ya jumla ya Dola za Kimarekani milioni 39, sawa na Sh. bilioni 98, inayotarajiwa kutekelezwa kuanzia mwaka 2025.

Dkt. Mwamba alibainisha miradi hiyo kuwa ni mradi wa kuanzisha chuo cha ufundi Morogoro, mradi wa kuimarisha huduma za mama na mtoto jijini Dar es Salaam, mradi wa kuanzisha mifumo ya usambazaji maji katika maeneo ya vijijini vya mkoa wa pwani na mradi wa kuanzisha mpango kabambe wa kitaifa wa barabara kuu na uboreshaji wa uwezo wa rasilimali watu.

Dtk. Mwamba aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Korea kupitia KOICA kwa kuunga mkono malengo hayo ambapo imekuwa mojawapo ya vyanzo vikuu vya ufadhili wa ruzuku katika kufanikisha miradi ya maendeleo na kusisitiza kuwa Tanzania itaendelea kuhakikisha kuwa rasilimali zote zinazopatikana kutoka KOICA zinatumika kwa uangalifu ili kufikia malengo yaliyokusudiwa ndani ya muda uliokubaliwa.

Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Korea (KOICA) Don Ho Kim, alisema kuwa Korea itaendelea kushirikiana na Tanzania katika maendeleo ya uchumi hasa katika ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji, afya pamoja na kuwezesha wafanyabiashara wadogo kuweza kunufaika na masoko.

Kuhusu miradi iliyowasilishwa na Tanzania alisema kuwa, ipo katika mchakato wa kuidhinishwa na Shirika hilo ambapo kati ya Novemba na Desemba mwaka huu inatazamiwa kuidhinishwa na Bunge la nchi hiyo, aliahidi nchi yake kuendeleza ushirikiano na kuunga mkono mipango ya maendeleo ya Tanzania
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, akimkabidhi zawadi yenye picha ya Mlima Kilimanjaro, Makamu wa Rais wa Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Korea (KOICA) anayeshughulikia mambo ya kimkakati, Mhe. Dong Ho Kim, baada ya kumaliza kikao kilichojadili ushirikiano na utekelezaji wa miradi ikiwemo ya miundombinu, elimu na afya, kilichofanyika jijini Dodoma.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba akizungumza kuhusu miradi ya maendeleo wakati wa kikao na Makamu wa Rais wa Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Korea (KOICA) anayeshughulikia Mambo ya Kimkakati Mhe. Dong Ho Kim, jijini Dodoma.
Makamu wa Rais wa Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Korea (KOICA), anayeshughulikia mambo ya kimkakati, Mhe. Dong Ho Kim, akizungumza wakati wa kikao na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba ambapo alisema kuwa Korea itaendelea kushirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa miradi mbalimbali, kilichofanyika jijini Dodoma.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, akiagana na Makamu wa Rais wa Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Korea (KOICA) anayeshughulikia mambo ya kimkakati, Mhe. Dong Ho Kim, baada ya kumaliza kikao kilichojadili ushirikiano wa maendeleo kati ya Tanzania na Korea katika utekelezaji wa miradi mbalimbali, kilichofanyika jijini Dodoma.
Ujumbe kutoka Tanzania ulioongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba (kushoto) na ujumbe kutoka Jamhuri ya Korea uliyoongozwa na Makamu wa Rais wa Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Korea (KOICA) anayeshughulikia mambo ya kimkakati, Mhe. Dong Ho Kim ukiwa katika mkutano ulioangazia ushirikiano wa maendeleo, kilichofanyika jijini Dodoma.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba (watano kulia), na Makamu wa Rais wa Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Korea (KOICA), anayeshughulikia mambo ya kimkakati, Mhe. Dong Ho Kim (wasita kushoto), wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wajumbe kutoka Wizara ya Fedha na ujumbe kutoka Korea (KOICA), baada ya kikao kilichojadili kuimarisha ushirikiano, kilichofanyika jijini Dodoma.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, WF, Dodoma)

Post a Comment

0 Comments