Ticker

6/recent/ticker-posts

HAKIELIMU NA ASASI ZA KIRAIA WAJA NA MKAKATl WA KUUNDA MAZINGIRA SALAMA SHULENI.

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

Zaidi ya asilimia 90 ya shule nne ambazo zimetumia Methodolojia ya Taasisi ya HakiElimu kwa lengo la kuunda mazingira ya shule kuwa mahali salama zimeachana na adhabu ya fimbo, ambapo imefanya wanafunzi kuwa karibu na walimu jambo ambalo limeboresha  masuala ya ufundishaji na kuleta matokeo chanya.

Hayo yamebainishwa leo Machi 21,2024 Jijini Dar es Salaam na Meneja Idara ya Utafiti, Uvumbuzi na Uchambuzi wa Sera- Hakielimu, Bw. Makumba Mwemezi wakati wa uzinduzi wa muungano wa asasi za kiraia zinazijuhusisha na utetezi wa haki za watoto.

Amesema mbinu hiyo imejaribiwa katika shule kutoka Kilwa, Masasi, Moshi pamoja na Korogwe ambapo imeibua matokeo chanya katika maeneo hayo na wameona ni vyema serikali ikatumia mbinu hiyo katika shule zote nchini.

Aidha Bw. Makumba amesema mbinu (Methodolojia) hiyo imelenga kuzibadilisha shule kuwa mahali salama, kwa kubadilisha mtizamo wa mwanafunzi na mwalimu kwa kuachana na suala la adhabu na kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia.

"Ni mbinu ambayo inautofauti na inafanya kazi, imejaribiwa Uganda na hapa kwetu tumejaribu katika maneneo hayo, kwahiyo tulikua tunabadilishana uzoefu kutoka maeneo ambayo tumeyaona". Amesema  

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo Cha mawasiliano Shirika la Msichana Initiative,Bi.Sarah Bedah ameeleza kuwa mtandao shule salama utawasaidia watoto kuwa salama shuleni,na kuwapa nguvu ya kusema aina mbalimbali ya matukio ya ukatili ambayo wanatendewa na kuyaona shuleni.

"Shirika la Msichana Initiative ambao ni moja ya wadau katika mtandao wa shule salama tumefungua madawati ya jinsia 29 kupitia klabu za shule ya msingi ambapo kupitia mtandao wa shule salama pia wanawasaidia watoto walio katika haya madawati mbinu ambazo tunazitumia zote ni sawa". Ameeleza Sarah

Naye Meneja Mkuu wa Shirika la Children Crossfire Bw. Heri Ayubu amesema taasisi yao ambayo inajishughulisha na suala la malezi pamoja na makuzi ya mtoto kuanzia umri 0 hadi miaka 8 imeona mambo mahimu yanayohitajika katika ukuaji  wa mtoto ni pamoja na afya,elimu,lishe,miongozo,Pamoja na suala la usalama.

Amesema sehemu ambayo mtoto yupo katika mazingira ya kulelea watoto na shuleni kuanzia umri wa miaka 0-18 anatakiwa kulindwa ili kumuepusha na vitendo vya ukatili na kutengeneza mazingira ambayo yataunda utimilifu wake akiwa mtu mzima na kuleta manufaa kwa taifa.

Mkutano huo unaoratibiwa na na Taasisi ya Haki Elimu umejumuisha Asasi za kiraia zaidi ya 15 zinazojihusisha na kutetea haki ya mtoto ambapo zimekutana kuunda nguvu za pamoja kutengeneza mazingira salama ya kujifunzia kwa wanafunzi na kujenga mahusiano bora yatakayoleta matokeo chanya.


Post a Comment

0 Comments