Na. John I Bera - Bagamoyo
Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imetoa mafunzo kwa waandishi wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET) kuhusu utoaji wa habari za utatuzi wa migongano baina ya Binadamu na wanyamapori huku ikiwataka waandishi hao kuzingatia weledi katika kuelimisha jamii hasa katika utoaji wa taarifa zinazohusiana na migongano baina ya Binadamu na Wanyamapori ili ziweze kuwasaidia waandishi hao waweze kutoa taarifa sahihi ambazo mwisho wa siku zitasaidia Taifa katika suala zima la uhifadhi.
Kauli hiyo imetolewa leo tarehe 22 Februari, 2024 na Mkuu wa Kitengo cha Mawailiano cha Wizara ya Maliasili na Utalii, Bw. John Mapepele alipokuwa akifungua Mafunzo ya siku mbili ya waandishi wa habari yaliyoaandaliwa na GIZ kupitia Mradi wa kutatua changamoto ya migongano baina ya binadamu na wanyamapori katika Ukanda wa Ruvuma Mkoa wa Lindi katika Wilaya ya Liwale na Ruvuma, Wilaya za Namtumbo na Tunduru kwa kushirikiana na Serikali, yaliyofunguliwa leo Bagamoyo mkoa wa Pwani.
Mapepele amesema kwa sasa wizara ina falsafa mbili kubwa ambazo ni uhifadhi na Utangazaji utalii na hivyo mafunzo hayo lengo lake kuu ni kusaidia katika kuimarisha uhifadhi ili usaidie katika utangazaji Utalii suala mabalo ni muhimu kwa jamii na Taifa kwa ujumla
"Uhifadhi ukiimarika mazao ya uhifadhi pia yataimarika kama vile utalii na hivyo kulifanya taifa kupata fedha za kigeni na kuimarisha uchumi wake kupitia hifadhi zetu." Alisema Mapepele
Ameongeza kuwa, Wizara imewekeza nguvu kubwa katika njia bora na za kisasa kutangaza Utalii na kuhifadhi huku akimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuimarisha uhifadhi ambapo amehakikisha uhifadhi unaendelezwa kwa ajili ya Vizazi vya sasa na vizazi vya baadae
Aidha, Mapepele amewataka wanahabari hao kutumia siku hizo mbili za mafunzo ambazo zitawasaidia wanahabari hao kujengewa uwezo kwa ajili ya kutoa habari za rasilimali zetu kwa faida ya Taifa kwa ujumla
“Niseme tu kwamba ni vizuri sana katika kipindi hiki sasa mbapo tutakuwa hapa kwa siku mbili tutumie fursa hii adhimu vizuri kwani itatusaidia sana kutujengea uwezo kwasababu katika nchi nyingi ambazo zimeendele hufanya haya tunayofanya leo’’ Alisema Mapepele.
Ameongeza kuwa nchi ya Tanzania ni moja ya nchi ambayo imepiga hatua kubwa katika eneo la uhifadhi ambapo asilimia 32 ya nchi imehifadhia jambo ambalo ni la kupongezwa.
Naye Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET), John Chikomo ameishukuru GIZ pamoja na Serikali kwa kuandaa mafunzo hayo ambayo kiujumla yatawasaidia waandishi hao kutoa Habari za migongano baina ya binadamu na wanyamapori kwa ufasaha na weledi mkubwa.
0 Comments