Ticker

6/recent/ticker-posts

TANAPA SIMAMIENI SHERIA KAMA ZILIVYOPITISHWA NA BUNGE MAJALIWA

Na. Richard Mrusha Katavi

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa (Mb) amewataka Makamanda wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kuratibu maeneo yao vizuri na kusimamia sheria za uhifadhi kama zilivyopitishwa na Bunge ili maliasilia zilizomo ziendelee kuleta tija kwa taifa.

Ameyasema hayo jana Februari 25.02.2024 aliposimama kuwasalimia wananchi wa kijiji cha Sitalike akiwa katika safari ya kikazi kuelekea kijiji cha Mpimbwe kilichopo Jimbo la Kavuu Mkoani Katavi.

Akiwa amesimama kusikiliza kero katika kijiji hicho cha Sitalike kilichopo mpakani mwa Hifadhi ya Taifa Katavi, wananchi walimuomba aseme neno ili wapate fursa ya kuvua samaki mto Katuma ambao unategemewa kwa zaidi ya asilimia 80 kiikolojia na uhai wa wanyama kama vile viboko na Mamba ambao maisha yao yote hutegemea maji ya mto huo.

Baada ya kusikiliza maombi hayo mhe. Majaliwa alisema, "Niwashukuru Makamanda wa TANAPA kwa kufanya maboresho katika eneo la mto Katuma, endeleeni kuratibu vizuri maeneo yenu na yale tuliyoyaweka kwenye sheria zetu yatekelezeni lakini pia fursa za wananchi nazo zipate nafasi ila si kwa kuingia katika maeneo yaliyohifadhiwa."

Wakati wote TANAPA kutaneni na wananchi, sikilizeni matamanio yao, waelimisheni juu ya namna watakavyonufaika na uhifadhi lakini pia waambieni na sheria zilizopo zifuatwe ili kuepusha misuguano."

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Nsimbo (CCM) Mhe. Annah Lupembe alisema kuwa suala la wananchi kuvua samaki mto Katuma lililoibuliwa hapa leo lilishapatiwa majibu katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini Sitalike - Katavi siku chache zilizopita ukiwahusisha wananchi wa Kata ya Sitalike, TANAPA na Mbunge. Ambapo TANAPA kwa kushirikiana na mbunge husika walikubaliana kuchukua hoja hiyo na kuiwasilisha ngazi za Wizara kwa hatua zaidi.

Naye, Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara - TANAPA Herman Batiho akiambatana na Kamanda wa Uhifadhi Kanda ya Kusini Steria Ndaga alisema, "Licha ya suala hili kushughulikiwa na mamlaka za juu tambueni kuwa, mto huu una mamba na viboko wengi, hivyo kuvua samaki eneo lenye wanyama wengi kiasi hicho ni kuhatarisha maisha yao aidha, kuna wanyama kama mamba na baadhi ya ndege hutegemea samaki hao. Pia kuna wavuvi wengine hutumia sumu na tumeshawakamata majangili wa hivyo. Sumu hii imekuwa na madhara makubwa kwa watumiaji wa samaki hao, viumbe vingine vinavyoishi majini na kwa wanyama wanaokunywa maji hayo".

Kamishna Batiho pia aliwataka wakazi wa Kata ya Sitalike na vijiji vinavyozunguka hifadhi ya Taifa Katavi kuachana na uvuvi wa kutegemea mto badala yake wachimbe mabwawa ya kufugia samaki TANAPA itashirikiana nao kwa kuwaletea wataalam watakaowafundisha namna bora ya kuchimba na kupata mbegu ya vifaranga.

Ikumbukwe kuwa Oktoba 10, 2019 aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli alipotembelea hifadhi hiyo aliiagiza TANAPA kuchimba mabwawa kunusuru uhai wa Viboko kutokana na kukauka kwa mto Katuma kulikosababishwa na matumizi yasiyoendelevu ya rasilimali maji. Hivyo kuruhusu matumizi holela ya mto huo yanaweza kuturudisha tena katika kadhia ya mwaka 2019.

Post a Comment

0 Comments