Ticker

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YAANZA UTEKELEZAJI MABORESHO YA RELI KANDA YA KASKAZINI.


Na Hamida Kamchalla, TANGA.


WIZARA ya Uchukuzi nchini pamoja na Wizara ya Uchukuzi, Mawasiliano na Usafirishaji ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimekutana jijini Tanga katika mkutano wa pili wa ushirikiano pamoja na kutembelea bandari ya Tanga.


Akiwa katika ziara ya kukagua bandari ya Tanga, Katibu Mkuu, Wizara ya Uchukuzi, Prof. Godius Kahyarara amesema kuwa serikali imeanza kutekeleza mradi maalumu wa kuboresha reli kutoka Dar es salaam kwenda Mikoa ya kaskazini ili kurahisisha usafiri kwa upande wa bandari nchini.


Prof. Kahyarara ameyasema hayo huku akiutaka uongozi wa bandari ya Tanga kutenga bajeti kwa mwaka huu ili kufanya maboresho ya reli inayoingia bandarini hapo, na kwamba mpango wa serikali ya awamu ya awamu ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuunganisha bandari nchini.


"Na hapa Tanga kuna mradi maalumu wa kufufua reli hii ya kaskazini kipande cha takribani km 435 kutoka Dar es salaam kwenda Mikoa ya kaskazini ambayo inapita hapa na tayari tumeshapewa fedha na serikali na maboresho yameanza kufanyika,


"Tumeshaanza kwa kung'oa vyuma vile iweze kuhimili mizigo mizito lakini poa na mwendo wa trend uongezeke, hii itafanya kuwa rahisi sana kuchukua mizigo kupeleka Dar na itakuwa msaada mkubwa kwa kuisadia bandari ya Dar es salaam" amesema.


Mbali na hilo pia ameutaka uongozi huo kuitangaza fursa za bandari ya Tanga badala ya kuangalia na kutangaza vitu vingine vilivyopo na kwa kuboresha reli usafiri wa kutoka Tanga kwenda Dar es salaam utakuwa ni rahisi.


Kwa upande wake Katibu Mkuu, Wizara ya Uchukuzi, Mawasiliano na Usafirishaji kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Khalifa Khamis Rajab amesema lengo la mkutano huo ni kuendeleza ushirikiano baina yao kwakuwa kazi inayotekelezwa ni moja katika kuwahudumia wananchi.


Naye Kaimu Meneja wa Bandari ya Tanga Peter Milanzi amesema matarajio ya kufunguka kwa Mkoa wa Tanga kupitia bandari hiyo ni makubwa na mradi wa uboreshaji umekamilika mwishoni mwa mwaka jana.


"Tunapokutana katika vikao vyetu huwa kuna baadhi ya vitu ambavyo vinaleta matatizo kati ya nchi hizo mbili, kwahiyo tunajadili na kuviweka sawa" amesema.


Pia Milanzi amefafanua kwamba tayari wameshaanza kupokea oda za kampuni kubwa kutoka nje ya nchi kutokana na uvoreshwaji mkubwa uliofanywa katika bandari hiyo.


"Mzigo mkubwa unaopita kwa sasa ni Amonium Nitrate, zao la mkonge, mafuta pamoja na malighafi za viwandani lakini pia mitambo ya viwanda hivyo, na timu yetu ya masoko inafanya kazi kubwa ya kuhakikisha wateja wanatumia bandari yetu ya Tanga' amesema.


Hata hivyo amesema serikali imefanya uwekezaji wa kuboresha bandari hiyo ili iweze kupokea meli gatini kwakuwa awali meli zilikuwa zikipakuliwa mizigo umbali wa km 1 na mita 700 kutoka kwenye gati hilo.


"Lakini pia serikali ililenga kuiwezesha bandari yetu kupokea mizigo mikubwa zaidi kwakuwa zamani ilikuwa ikihudumia mizigo mpaka tani laki 7.5 lakini kwa uwekezaji huu sasa tunaweza kuhudumia tani milioni 3 kwa mwaka" amesema.


Kuhusu suala la reli iliyoingia bandarini hapo Milanzi alisema, "reli inaingia lakini kutokana na huu mradi uliofanyika kuna baadhi ya vipande viliondolewa lakini makubaliano ya uboreshaji yameshafanyika kati ya TRC na bandari" amesema.

Post a Comment

0 Comments