Ticker

6/recent/ticker-posts

RAIS SAMIA ARIDHIA KUANZISHWA KWA MTAALA WA MASOMO YA UTALII

Na Happiness Shayo-Dodoma

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameridhia kuanzishwa kwa masomo ya Utalii kwa kidato cha tano na sita nchini lengo ikiwa ni kuendelea kuikuza Sekta ya Utalii.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) katika kikao kati yake na Wabunge wa Mikoa ya Kilimanjaro na Tanga kilichofanyika ukumbi wa Utawala Bungeni jijini Dodoma leo.

“Tunashukuru Mheshimiwa Rais aliona umuhimu wa kuanzishwa kwa mchepuo wa masomo ya utalii na hakuchukua muda mrefu kulikubali suala hilo” Mhe. Kairuki amesisitiza.

Amesema lengo la kuanzishwa kwa mchepuo wa masomo ya utalii ni kuendelea kuiboresha sekta hiyo akitolea mfano kutoa mafunzo ya utoaji wa huduma kwa wateja, lugha na kadhalika.

Amesema ameshawasilisha toolkit ya mchepuo huo ambayo inaendana na matakwa ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani ( World Tourism Organization-UNWTO)pamoja na Wizara ya Elimu na kwamba kilichobaki ni maandalizi ya awali kwa ajili ya utekelezaji.

Aidha, katika kuboresha utoaji wa huduma kwa watalii, amesema Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) kimeanza kutoa mafunzo kwa watendaji wa sekta mbalimbali wanaohusika na utoaji huduma ikiwa ni pamoja na Uhamiaji, Askari Polisi na watumishi wa sekta ya utalii.

Pia, amesema amefanya maongezi na taasisi ya Mastercard Foundation kwa ajili ya kutoa mafunzo ya utoaji huduma na lugha ili wawe na ujuzi wa jumla na kuweza kuyazungumzia ipasavyo maeneo yao.

Kuhusu utangazaji utalii Waziri Kairuki amesema kuwa mazungumzo na taasisi mbalimbali yameshafanyika ili kushirikiana katika kutangaza utalii akitolea mfano mashirika ya ndege ya Saudia Airline,Turkish Airline, Air Tanzania Company Limited na Shirika la Kiserikali la CTG la China ambapo limeonesha nia ya kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania.

Katika hatua nyingine, Waziri Kairuki ameahidi kufanyia kazi mapendekezo yote katika Sekta ya Utalii ya kutangaza zaidi vivutio vya utalii, kuboresha miundombinu ya maeneo ya hifadhi, kushughulikia changamoto za wanyamapori wakali na waharibifu pamoja na masuala ya kifuta jasho /machozi.

Post a Comment

0 Comments