Ticker

6/recent/ticker-posts

MKOA WA TANGA WAKABIDHIWA VIFAA KWA AJILI YA UTOKOMEZAJI MAGONJWA VVU NA KIFUA KIKUU


Na Hamida Kamchalla, TANGA.

KATIKA kuhakikisha huduma za afya zinaboreshwa nchini, vifaa vyenye thamani ya sh milioni 800 vimekabidhiwa mkoani Tanga katika hospitali ya Rufani Bombo ili kusaidia kusambaza na kuhifadhi sampuli za damu katika vituo vilivyo mbali na mji.

Vifaa hivyo vimekabidhiwa na Shirika la Tanzania Health Promotion Support (THPS) kwa udhamini wa serikali ya Marekani kupitia kituo chake cha kudhibiti na kupambana na magonjwa, (CDC), ambavyo vitasaidia zaidi kwa wenye maambukizi ya vvu pamoja na kifua kikuu.


Akiongea kwenye hafla hiyo, Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema katika kuhakikisha huduma za afya zinaboreshwa, serikali kwa kushirikiana na serikali ya Marekani, kupitia Shirika la (THPS), imeweka nguvu kubwa kwenye mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI kwa kutumia mbinu mbalimbali.


"Lengo kubwa ni kudhibiti maambukizi mapya, kuibua wote wenye maambukizi na kuwapatia matibabu waimarike na wafikie kiwango cha kufubaza virusi ili waweze kuishi maisha yao ya kawaida na kujenga uchumi,


"Napenda kutoa shukrani za dhati kwa wadau wote kwenye sekta ya afya wanaounga mkono juhudi za serikali kwenye mapambano dhidi ya UKIMWI, tunaomba muendelee na juhudi hizi na sisi tuko tayari kuwapa ushirikiano wa kutosha" amesema.


Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la THPS, Dkt. Redempta Mbatia amesema mbali ya kutoa msaada huo, pia wanatengeneza mpango kazi wenye bajeti ya zaidi ya sh bilioni 6 ambazo zitatumika kugaramia utoaji wa huduma mbalimbaliza kinga, matunzo na matibabu kwa Mkoa wa Tanga kwa mwaka wa kwanza wa fedha.


"Pia tumetenga sh bilioni 4.886 ambazo zitatumika moja kwa moja mkoani hapa kwa ajili ya kugaramia vipaumbele vyake, ikiwemo kuajiri watumishi wa huduma za afya,


"Zaidi tumesha ajiri watumishi wa ziada 658 kupitia ofisi za wakurugenzi wa halmashauri ambao wanalipwa ujira kupitia fedha za mfadhili" amesema Dkt. Mbatia.


Alivitaja vifaa hivyo kuwa ni pamoja na pikipiki 50, friji 72 za kuhifadhia sampuli katika vituo vya afya, centrifuges 56 za kuchakata sampuli hizo, kompyuta 50, UPS 50 na printer 50 kwa ajili ya kuweka taarifa za wapojea huduma.


"Leo tunakabidhi vifaa hivi ambavyo vimegarimu takribani sh milioni 800, na vinategemewa kuboresha huduma za afya kwa wakazi wa Mkoa wa Tanga na vimetolewa na walipa kodi wenzetu wa Marekani ambao wamejito ili kuwezesha utoaji huduma bora, kudhibiti na kuokoa maisha,


"Wito wetu ni kwa watendaji watakaoviyumi au kuvisimamia, wavitunze ikiwemo kuvifanyia matengenezo kinga kwa wakati na tunaahidi kuendelea kushirikiana bega kwa bega katika kuunga mkono juhudi za serikali,


"Nishukuru sana serikali hii ya awamu ya sita, imeweka misingi imara ya Kitaifa na Kimataifa, utendaji kazi na utoaji huduma za afya, tukumbuke kuwa kama siyo sera madhubuti ya nchi yetu, hata ufadhili huu tusingeupata" alibainisha.


Mkurugenzi wa Mradi, Kituo cha Marekani cha Kuzuia na Kuzuia na Magonjwa (CDC), Dkt. George Mgomella amesema vifaa hivyi vimegarimu sh bilioni 800 sawa na dola za Kimarekani 300 ni maalumu kwa ajili ya magonjwa ya VVU na kifua kikuu.


Pia amesisitiza kuwa watendaji wanapaswa kuvitunza na kuvifanyia matengenezo kwa wakati vifaa hivyo ili kufikia lengo lililokusudiwa na kutokomeza magonjwa hayo hayo ifikapo mwaka 2030.

Post a Comment

0 Comments