Ticker

6/recent/ticker-posts

MAPATO YA UTALII, MADINI, VIWANDA YAVUNJA REKODI CHINI YA RAIS SAMIA

 

 

*Mapato ya utalii, madini, viwanda yavunja rekodi chini ya Rais Samia

* Utalii na dhahabu zaingiza Shilingi trilioni 8 kwa kila sekta kwa mwaka kwa mara ya kwanza

* Mauzo ya bidhaa nje ya nchi sasa ni zaidi ya Shilingi trilioni 18 kwa mwaka

* Sera za uchumi za Rais Samia zaleta mageuzi makubwa nchini


Februari 19, 2024

Na Mwandishi Wetu - Dar es Salaam

Sera za uchumi za Rais Samia Suluhu Hassan zimeleta mageuzi makubwa nchini, huku sekta za utalii, madini na viwanda zikivunja rekodi kwa kuingiza mapato makubwa zaidi tangu Tanzania ipate uhuru.

Baada ya Rais Samia kuingia madarakani Machi 2021, mabadiliko makubwa yameanza kuonekana kwenye uchumi.

Chini ya Rais Samia, jumla ya mauzo ya nje ya bidhaa za Tanzania (exports) yameongezeka na kuvuka Dola za Marekani bilioni 7 (Shilingi trilioni 18) kwa mwaka kwa mara ya kwanza.

Mauzo ya nje yamevunja rekodi hiyo ya kuvuka Dola bilioni 7 kwenye miaka miwili mfululizo, yaani mwaka 2022 na mwaka 2023.

Kabla ya Rais Samia kuingia madarakani, mauzo ya nje ya Tanzania yalikuwa chini ya Dola za Marekani bilioni 7 kwa mwaka.

Sekta ya utalii imevunja rekodi mwaka jana kwa kuingiza Dola za Marekani bilioni 3.36 (Shilingi trilioni 8.7), ikiwa ni ongezeko kutoka Dola za Marekani bilioni 2.52 mwaka 2022.

Hii ni mara ya kwanza katika historia ya nchi kwa utalii kuingiza zaidi ya Dola bilioni 3 kwa mwaka, kwa mujibu wa ripoti mpya ya kila mwezi ya Benki Kuu ya Tanzania (monthly economic review). 

Tanzania ilipokea jumla ya watalii 1,808,205 mwaka jana, ikiwa ni idadi kubwa kuwahi kufikiwa katika historia ya nchi.

Ukuaji mkubwa wa utalii umetokana na jitihada za Rais Samia kukuza sekta hiyo, ikiwemo ushiriki wake kwenye filamu ya Royal Tour.

Kwa upande wa madini, mauzo ya nje ya dhahabu yaliingiza Dola za Marekani bilioni 3.05 mwaka 2023, kutoka Dola bilioni 2.83 kwa mwaka 2022 na kuvunja rekodi kwa kuvuka Dola bilioni 3 kwa mara ya kwanza.

Kwa upande wa sekta ya viwanda, mauzo ya nje ya bidhaa za viwandani yamevuka Dola za Marekani bilioni 1 (Shilingi trilioni 2.6) kwa mwaka kuanzia mwaka 2021.

Kabla ya Rais Samia kuingia madarakani, mauzo ya nje ya bidhaa za viwandani za Tanzania yalikuwa chini ya Dola za Marekani bilioni 1 kwa mwaka.

Ripoti za fedha za mabenki za robo ya mwisho ya mwaka jana (Q4 2023) nazo zimeonesha kuwa benki za biashara mwaka jana zilivunja rekodi ya mapato na faida.

Mageuzi yaliyofanywa na Rais Samia ni pamoja na kuimarisha mazingira ya biashara nchini, kuweka sera nzuri kwa sekta binafsi na kuagiza Mamlaka ya Mapato ya Tanzania (TRA) itumie njia rafiki za kukusanya kodi badala ya ubabe.

Post a Comment

0 Comments