Ticker

6/recent/ticker-posts

MABAKI YA MKONGE HUZALISHA PROTINI NA MBOLEA - UTAFITI.


Na Hamida Kamchalla

Imezoeleka mkonge baada ya kuchakatwa na kupatikana singa, mabaki yake hutupwa kama uchafu kwa kuwa hayana matumizi mengine.
Hatua hiyo ni tofauti kwa mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu (PhD), katika Chuo Kikuu cha Afrika cha Nelson Mandela cha Sayansi na Teknolojia (NM-AIST) kilichopo mkoani Arusha, Aziza Konyo ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).

Konyo amefanya utafiti na kuzalisha nzi chuma na mbolea kwa kuongeza thamani kwa kutumia mabaki hayo ya mkonge.

Akizungumza baada ya kikao cha uwasilishaji wa ugunduzi wa utafiti huo, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), Saddy Kambona amesema utafiti huo ambao umesajiliwa kwa hati miliki pia umebaini licha ya kuzalisha nzi chuma hao ambao hutumika kama protini kwenye chakula cha mifugo lakini pia mabaki ya chakula wanachokula ni mbolea nzuri inayotumika katika mazao mbalimbali.

“Bodi imepokea wasilisho la utafiti huo na imefurahi kuona kwamba zao la mkonge linazidi kupata thamani kwa sababu tumezoea baada ya kupatikana singa basi kinachobaki chote ni uchafu kinatupwa,

“TSB ina mahusiano ya muda mrefu na Chuo cha Nelson Mandela katika kufanya tafiti mbalimbali kuhusu uongezaji thamani wa zao la mkonge,

"Kwa hiyo Aziza Konyo chini profesa wake Anthony Mshandete na Revocatus Machunda amefanya utafiti wa kuzalisha nzi chuma kutokana na mabaki ya mkonge ambayo hutumika kama protini kwenye chakula cha mifugo jamii ya ndege wanyama na binadamu,” amesema Kambona.

Utafiti huu ni wa pili kufanyika na chuo hicho ambapo utafiti wa kwanza unatekelezwa na chuo hicho kwa ushirikiano na Serikali ya Denmark kupitia Shirika lake la Maendeleo (Danida), ambapo umejikita katika maeneo matatu ambayo ni uzalishaji gesi asilia, ujenzi na kile kitakachozalishwa kutokana na gesi asilia.

Post a Comment

0 Comments