--Zaidi ya Wataalam 6 wa GST Wanufaika na Mafunzo ya Utafiti wa Visawe Mbali
Cape Town
Wataalam kutoka Taasisi ya Japan Organisation for Metals and Energy Security (JOGMEC) inayojishughulisha na Utoaji Mafunzo ya Utafiti wa Madini kwa kutumia njia ya Visawe Mbali (Remote Sensing Technology) ya nchini Japan hivi karibuni ilionesha nia ya kushirikiana na Tanzania kuziwezesha kampuni za nchi hiyo zinazojishughulisha na utafiti wa Madini Mkakati nchini.
Hayo yalijiri wakati Tanzania ikishiriki katika Mkutano wa Mining Indaba uliofanyika nchini Afrika Kusini kuanzia tarehe 5 hadi 8 Februari, 2024 ambapo Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa ulipata wasaa wa kukutana na wadau mbalimbali wenye nia ya kuwekeza na kupata taarifa za kina kwenye fursa walizolenga kuwekeza katika Sekta ya Madini nchini.
Katika kikao hicho, JOGMEC ilieleza maeneo ya ushirikiano kwa kampuni za Japan kuwa ni uendelezaji wa madini mkakati ikiwemo copper, nickel, lithium, colbat na manganese ambayo nchi ya Japan ina mahitaji makubwa ya madini hayo. Kutokana na mahitaji makubwa ya madini hayo duniani kuongezeka, inaelezwa kuwa, ifikapo mwaka 2050 mahitaji yake yatafikia tani milioni 150.
Katika Mkutano wa Indaba Tanzania iliweka vipaumbele kutangaza fursa za uwekezaji katika maeneo ya utafiti, utoaji huduma migodini, uchimbaji madini na uongezaji thamani madini ambapo ilitumia mktano maalum wa Tanzania kutangaza fursa zake, midahalo, vikao vya ana kwa ana na maonesho kutangaza uwepo wa fursa za kiuwekezaji katika sekta ya madini kupitia maeneo husika.
Katika kikao hicho, Dkt. Kiruswa aliueleza ujumbe huo kuhusu utayari wa Tanzania kushirikiana na kampuni hiyo kupitia kupitia taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST).
"Tuko tayari kuwapokea na kufanya makubaliano kupitia taasisi yetu ya GST,’’ alisema Dkt. Kiruswa.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa GST Dkt. Mussa Budeba alisema kuwa, kumekuwepo mahusiano ya muda mrefu na taasisi hiyo kupitia mafunzo ya utafiti wa madini kwa kutumia teknolojia ya visawe mbali ambapo zaidi ya watalaam sita (6) tayari wamenufaika na program ya mafunzo kutoka JOGMEC.
Mwaka 2024, Tanzania imeshiriki kwa Pamoja katika Mkutano wa Mining Indaba kwa kushirikiana na Sekta binafsi chini ya mwanvuli wa Chemba ya Migodi Tanzania ambapo zaidi ya washiriki 100 kutoka Tanzania walishiriki katika mkutano huo mkubwa unaofanyika kila mwaka nchini humo.
#TANZANIA@The Mining Indaba2024 #InvestInTanzaniaMiningSector
0 Comments