Ticker

6/recent/ticker-posts

BASHUNGWA AIAGIZA TBA KUSHUSHA RUNGU KWA TAASISI ZA SERIKALI NA WATUMISHI WANAODAIWA

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameuagiza Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), kuelekeza nguvu ya ukusanyaji wa kodi ya pango na majengo kwa Wizara, Taasisi na Watumishi waliopanga kwa Wakala huo ambao wamekuwa wakisuasua kulipa madeni hayo kwa wakati.

Ametoa agizo hilo jijini Dodoma katika kikao cha uwasilishaji wa madai na madeni ya TBA, ambapo amesisitiza zoezi la Awamu ya pili linaloendelea lilete matokeo mazuri zaidi ya ile ya awali ili fedha zinazopatikana zisaidie katika utekelezaji wa miradi mingine.

“Niwapongeze kwa jitihada kubwa mliyoifanya katika ukusanyaji wa madeni Awamu ya Kwanza, Hivyo endeleeni na nguvu ile ile katika Awamu ya Pili, matarajio yangu nikuona madeni ya TBA yanakwisha”, amesisitiza Bashungwa.

Bashungwa ameitaka TBA kuhakikisha unayaangalia kwa karibu na kuyaendeleza maeneo yake katika sehemu mbalimbali nchini ili kuepusha migogoro ya ardhi inayojitokeza katika maeneo hayo kutokana na uvamizi.

Aidha, Bashungwa ameutaka uongozi wa Wizara ya Ujenzi kushirikiana kwa karibu na TBA katika ukusanyaji wa madeni ili kuongeza ufanisi na tija katika zoezi hilo.

Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi Eng. Aisha Amour, ameitaka TBA kuweka utaratibu mzuri wa ulipaji wa kodi na kukumbusha madeni mara kwa mara kwa wapangaji wake ili kutolimbikiza madeni hayo na mpangaji kushindwa kulipia kwa wakati.

Akitoa taarifa, Mtendaji Mkuu wa TBA, Arch. Daud Kondoro, ameeleza kuwa kuanzia mwezi Julai – Disemba, 2023 Wakala huo uliajiri Dalali ambaye alianza kukusanya madeni katika mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Arusha na Tanga ambapo jumla ya takribani Shilingi Bilioni 21 zilikusanywa.

“Katika makusanyo hayo kiasi cha Shilingi Bilioni 7 .9 kilitokana na kodi ya pango na mauzo wakati kiasi cha Shilingi Bilioni 13 kilitokana na mapato mengine”, amefafanua Arch. Kondoro.

Tangu kuanza zoezi la ukusanyaji wa kodi Wakala umekuwa na taratibu ya kuunda timu za kufuatilia madeni ambazo hukutana na washitiri kuwakumbusha madeni yao na kupanga mkakati wa kulipa.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, akisisitiza jambo katika kikao kazi cha uwasilishaji wa madai na madeni ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), kilichofanyika Februari 8, 2024 jijini Dodoma.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi, Eng. Aisha Amour akizungumza katika kikao kazi cha uwasilishaji wa madai na madeni ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), kilichofanyika Februari 8, 2024 jijini Dodoma.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Arch. Daud Kondoro, akitoa taarifa ya madai na madeni katika kikao kazi cha uwasilishaji wa madai hayo kilichofanyika Februari 8, 2024 jijini Dodoma.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ufundi na Umeme kutoka Wizara ya Ujenzi, Qs. Nyaswa Machibya, akifafanaua jambo katika kikao kazi cha uwasilishaji wa madai na madeni ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), kilichofanyika Februari 8, 2024 jijini Dodoma. Kushoto kwake ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Ludovick Nduhiye.

PICHA NA WU


Post a Comment

0 Comments