Kamanda wa polisi Mkoa wa Tanga ACP Almachius Mchunguzi amesema mnamo februari 27, majira ya saa 7 mchana, maeneo ya kona ya Msimbazi, Wilaya ya Korogwe katika barabara kuu ya Segera- Bwiko lilitokea tukio la wananchi kuchoma moto basi.
Amebainisha kuwa gari namba T. 668 BCD, Scania, mali ya kampuni ya Saibaba likiendeshwa na Seasa Chuwa (48), likitokea Dar es salaam kuelekea Arusha liligongana na pikipiki namba MC 819- EAF, aina ya Haojue iliyokuwa ikiendeshwa na Awadhi Juma (20) mkazi wa Mtonga, Korogwe.
"Ajali hiyo ilisababisha majeruhi kwa dereva wa pikipiki na uharibifu wa gari, baada ya ajali kundi la watu waliokuwa wakiendesha pikipiki walifika eneo la tukio kwa lengo la kufanya uhalifu, ikiwemo kuiba mizigo ya abiria na mali zao" amebainisha.
Kamanda Mchunguzi amesema, baada ya wahalifu hao kugundua kuwa polisi wanakaribia kufika kwa ajili ya uokozi waliamua kulichoma gari hilo ambalo liliteketea kwa moto.
Pia amebainisha kwamba katika ajali hiyo hakuna madhara kwa binadamu yaliyojitokeza, "uchunguzi umefanyika na mpaka sasa watuhumiwa 13 wamekamatwa kuhusiana na tukio hilo na mara uchunguzi utakapokamilika watafikishwa mahakamani".
Kamanda amesema jeshi hilo mkoani humo linaendelea kutoa wito kwa baadhi ya wananchi ambao wanaendelea kujihusisha na vite do vya uhalifu kuacha kwani halitasita kuwakamata na kuwafikisha mahakamani.
"Jeshi la polisi pia, linalaani vikali tabia za wananchi kujichukulia sheria mikononi kwa visingizio vya hasira kali ambavyo ni kinyume na sheria na halitasita kuwachukulia hatua kali,
"Aidha tunatoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na polisi katika kubaini na kuzuia uhalifu ili Mkoa wetu wa Tanga uendelee kuwa na amani na usalama wa kutosha" amesema.
Wakati huo huo, Kamanda Muchunguzi amesema jeshi hilo limepokea taarifa ya kutekwa kwa Buki Kizigina, mkazi wa Tanga na baada ya uchunguzi ilibainika anayetuhumiwa kumteka ni mkazi wa Kimara Tanesco, jijini Dar es salaam.
Kamanda amefafanua kwamba uchunguzi umebaini kuwa mtuhumiwa aliyetambulika kwa majina ya Khalid Mwarangi akiwa na wenzake wawili walimteka Kizigina mnamo februari 12 mwaka huu na kumficha maeneo mbalimbali kwa kumuhamisha toka eneo moja kwenda jingine ndani ya jiji la Tanga.
"Watuhumiwa walidai kupatia kiasi cha sh milioni 50 au warejeshewe dawa za kulevya walizompa asafirishe kwa ajili ya kwenda kuuza, lakini matokeo yake aliporudi kutoka nchini Ethiopia, aliwaeleza kuwa alikamatwa akiwa nchini humo,
"Uchunguzi unaendelea ili kukusanya ushahidi zaidi kwani hata wakati mtuhumiwa mmoja anakamatwa alikutwa na gramu 25 za dawa zinazodhaniwa ni za kulevya pamoja na hati mbili za kusafiria" amesema.
0 Comments